1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benedikti wa 16 aacha nafasi wazi kwa Papa mpya

1 Machi 2013

Kiti cha Papa kiko wazi kuanzia leo Ijumaa hadi atakapochaguliwa Papa mpya. Benedikt wa 16 aliondoka kwenye makazi ya Papa jana, na kutangaza kwamba anaenda kuanza safari ya mwisho ya maisha yake akiwa hujaji wa kawaida.

Benedikt wa 16 ameacha nafasi wazi kwa mtu atakayechaguliwa kuwa mrithi wake.
Benedikt wa 16 ameacha nafasi wazi kwa mtu atakayechaguliwa kuwa mrithi wake.Picha: Reuters

Siku ya mwisho ya Benedikt 16 kama Papa jana Alhamis ilikuwa yenye hisia kubwa. Walinzi wa Papa, Swiss Guards waliiziba milango ya nyumba mpya atakakoishi Benedikt, na waliitelemsha bendera ya Vatican kama ishara ya kumalizika kwa jukumu lao kumlinda Papa. Mshale wa saa ulipokaribia saa mbili usiku, muda rasmi wa kujiuzulu kwa Papa, umati wa watu waliokusanyika nje walipaza sauti zao wakimtakia maisha marefu Benedikt wa 16. Miongoni mwa watu waliokuja kumuaga papa ni rais Dilma Rousseff wa Brazil, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wakatoliki ulimwenguni.

Akizungumza baada ya safari fupi ya helikopta kutoka Vatican hadi makazi yake mapya, Benedikt wa 16 alisema kwamba yeye siye papa tena, bali hujaji wa kawaida. Na alipokuwa akiwaaga makardinali jana alisema, ''Miongoni mwenu kuna papa wa siku zijazo, na ninatoa ahadi ya kumwenzi na kumheshimu bila masharti yoyote.''

''Miongoni mwenu kuna atakayechaguliwa na mungu kuchukua nafasi yangu'' Benedikt wa 16 aliwaambia makardinali hawa.Picha: PATRICK HERTZOG/AFP/Getty Images

Rais Rousseff alimpongeza Benedikt wa 16 kwa uamuzi wake, na kumshukuru kwa kumtakatifuza raia wa Brazil. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alihudhuria misa maalumu mjini Berlin, iliyoandaliwa kuadhimisha siku ya mwisho ya benedikt wa 16 akiwa na wadhifa wa Papa. Katika kanisa la Mtakatifu Patrick mjini New York, mamia ya waumini walikusanyika kutoa heshima kwa papa huyo aliyestaafu.

Vatican imesema kuwa leo hii itatuma barua ya mwaliko rasmi kwa makardinali kushiriki katika mfululizo wa mikutano itakayoanza wiki ijayo, ambayo itapanga tarehe ya kikao cha kumchagua Papa mpya. Katika mikutano hiyo makardinali watabainisha masuala ya kipaumbele kwa kanisa katoliki baada ya miaka minane chini ya uongozi wa Benedikt wa 16, ambao ulighubikwa na mivutano ya ndani na kashfa za makasisi waliohusika na visa vya kuwanajisi watoto.

Mchakato wa kumchagua papa mpya utaanza mnamo nusu ya kwanza ya mwezi huu wa Machi, na mamilioni ya wakatoliki ulimwenguni wanatazamia kuwa mtu atakayechaguliwa kuliongoza kanisa ataleta ahueni katika kanisa hilo linalokabiliwa na changamoto kubwa ya kupotea kwa imani miongoni mwa wakazi wa nchi za magharibi, huku wakristu wakikabiliwa na ubaguzi katika baadhi ya nchi.

Helikopta iliyomsafirisha Benedikt wa 16 kutoka Vatican.Picha: Getty Images

Benedikt wa 16 ni Papa wa pili kujiuzulu katika historia ya miaka 2000 ya kanisa. Ataendelea kuitwa baba mtakatifu na kubakia na jina lake la upapa la Benedikt wa 16, akiitwa papa mstaafu.

Benedict wa 16 amehamia katika kasri ya Gandolfo nje kidogo ya mji wa Roma na kukaa huko kwa miezi miwili, kabla ya kurudi Vatican na kuishi katika nyumba ya kitawa hadi kifo chake.

Maswali yanaulizwa kuhusu hali isiyokuwa ya kawaida ya mapapa wawili kuishi katika eneo moja, lakini msemaji wa Vatican Federico Lombardi amesema hakuna haja ya maswali hayo, kwani Benedikt wa 16 hana nia ya kuingilia kwa hali yoyote ile kazi ya mtu atakayechaguliwa kuwa papa mpya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/DW online

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW