1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benin na Chad zafanya uchaguzi uliosusiwa na upinzani

Babu Abdalla12 Aprili 2021

Raia wa Chad wamepiga kura katika uchaguzi wa Urais jana Jumapili huku Idriss Deby Itno akielekea kushinda muhula wa sita madarakani.

Benin | Präsidentschaftswahl 2021 | Stimmauszählung Cotonou
Picha: Séraphin Zounyekpe/DW

Raia wa Chad wamepiga kura katika uchaguzi wa Urais jana Jumapili huku Idriss Deby Itno akielekea kushinda muhula wa sita madarakani, na nchini Benin Rais Patrice Talon anaelekea kuchaguliwa tena baada ya uchaguzi wa Jumapili uliokumbwa na madai ya wizi wa kura.

Mshirika muhimu katika kampeini ya kupambana na wapiganaji wenye itikadi kali katika eneo la Sahel, Deby mwenye umri wa miaka 68, ndiye mgombea anaepewa nafasi kubwa zaidi kuibuka na ushindi kati ya wagombea sita kufuatia kampeni ya kisiasa ambamo maandamano yalipigwa marufuku.

Soma zaidi: Benin wafanya uchaguzi kukiwa na wasiwasi

Swali kuu ambalo limejitokeza kuhusu uchaguzi huo ni juu ya idadi ya waliojitokeza kupiga kura, baada ya baadhi ya wapinzani kutaka kususiwa kwa uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema jana Jumapili baada ya kupiga kura katika mji mkuu wa N'Djamena, Deby alitoa wito kwa raia wa Chad kujitokeza kwa wingi na kupiga kura.

Kulikuwepo na idadi kubwa ya vikosi vya usalama katika mji huo mkuu, huku ukosefu wa vifaa vya kupigia kura ukichelewesha kufunguliwa kwa vituo vingi vya kupigia kura.

Katika wilaya ya Moursal, inayotajwa kuwa ngome ya upinzani, afisa mmoja wa uchaguzi amesema kuwa "wapiga kura watatu tu" ndio waliofika katika kituo cha kupigia kura tangu kilipofunguliwa.

Kufikia Jumapili jioni, vituo vya kupigia kura vilikuwa vimefungwa huku zoezi la kuhesabu kura likiendelea. Matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa mnamo Aprili 25, huku matokeo ya mwisho yakitarajiwa kutangazwa mnamo Mei, 15.

Marekani imesema inafuatilia uchaguzi wa Chad

Rais wa Benin Patrice TalonPicha: Rodrigue Guézodjè/DW

Alhamisi iliyopita, Marekani iliwataka wasimamizi wa uchaguzi wa Chad na mahakama nchini humo kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa njia huru na haki. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price alisema Marekani itakuwa inafuatilia uchaguzi huo.

Wakati hayo yakiarifiwa, nchini Benin Rais Patrice Talon anaonekana kuelekea kuchaguliwa tena.

Talon, ambaye amejipatia utajiri wake kupitia biashara ya pamba alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016, alikabiliana na wapinzani wawili wanaotajwa kuwa dhaifu wakati viongozi wengine wakuu wa upinzani wakisusia uchaguzi huo.

Hali ya wasiwasi iliibuka kuelekea kwa uchaguzi huo wa Jumapili. Maandamano yaliripotiwa katika miji kadhaa inayotajwa kuwa ngome za upinzani japo zoezi la upigaji kura liliendelea kwa amani katika sehemu nyengine.

Ernest Bai Koroma, Rais wa zamani wa Sierra Leone na msimamizi wa uchaguzi wa kanda ya mataifa ya Afrika Magharini ECOWAS, alisema jana ilikuwa bado mapema kufanya hitimisho lolote kuhusu zoezi la uchaguzi.

Wahimizao maandamano ya amani Chad

03:27

This browser does not support the video element.

"Vifaa vya kupigia kura na vituo vya kupigia kura, kwa vile ambavyo tumevitembelea, vilifunguliwa kwa wakati na maafisa wa uchaguzi walikuwepo. Zoezi linaendelea japo ni mapema mno kuamua hasa idadi ya wapiga kura watakaojitokeza lakini tunafuatilia zoezi lenyewe"

Nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, wakati mmoja iliwahi kusifika kama nchi yenye demokrasia imara japo sasa hali imebadilika. Idadi kubwa ya wapinzani wameikimbia, wengine wamezuiwa kuwania nafasi za uongozi ilhali wengine wamelengwa kwa uchunguzi na mahakama maalum.

Zaidi ya watu milioni 4.9 wamesajiliwa kama wapiga kura. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa aidha leo Jumatatu au kesho Jumanne.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW