Benin: Uchaguzi wa Bunge kufanyika tarehe 28.04.2019
26 Aprili 2019Watu wa Benin wataamua hapo kesho juu ya bunge jipya katika uchaguzi unaofanyika bila ya vyama muhimu vyaupinzani kushiriki. Rangi za vyama vinavyoegemea upande wa serikali ndizo zinazong'ara kwenye mitaa ya mji mkuu, Cotonou. Kijani ya chama cha Republican na manjano ya chama cha Progressive Union. Ni vyama hivyo viwili tu vinavyoshiriki katika uchaguzi huo.
Makamu wa spika wa bunge Eric Houndete ambae pia mwanachama wa chama cha upinzani amesema kinachotokea ni hadaa, amesema huo si uchaguzi. Houndete ameeleza kuwa rais amevitayarisha vyama viwili vilivyomo kwenye mfungamano wake wa kisiasa. Matokeo yake ni kwamba ni chama kimoja tu kinachoshiriki katika uchaguzi huo wa bunge.
Kwa mujibu wa ripoti ya jarida maarufu la Forbes iliyochapishwa manmo mwaka 2015 rais wa Benin Patrice Talon alikuwa na utajiri wa dola milioni 400. Aliingia madarakani mnamo mwaka 2016 baada ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi. Wanaomuunga mkono wanasema rais huyo ataleta mageuzi makubwa nchini Benin.
Rais Patrice Talon anahamasishwa na rais Paul Kagame na anasifu ufanisi wa kazi wa rais huyo wa Rwanda. Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanalalamika juu ya utawala wake wa kidikteta. Asasi hizo zinadai kwamba Kagame anatumia nguvu kuwanyamazisha wapinzani.
Nchini Benin ni tume huru ya uchaguzi inayoamua juu ya vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi. Tume hiyo ya kitaifa ilivinyima ruhusa ya kushiriki katika uchaguzi wa bunge vyama vitano, ikiwa pamoja na kile cha rais wa hapo awali Bini Yayi.
Tume ya uchaguzi imesema iliupitisha uamuzi huo mapema mwezi huu kwa sababu vyama hivyo havikujiandikisha namna inavyostahili na pia kwa sababu havikulipa kodi. Mwakilishi wa wakfu wa Friedrich Ebert nchini Benin Hans-Joachim Preuß amesema inaonekana wazi kwamba ni vyama vya upinzani tu ambavyo vimekataliwa kushiriki katika uchaguzi.
Tume ya uchaguzi imejenga urasimu wa kiwango kikubwa kwa kubadilisha sheria ya uchaguzi. Ni vyama vya serikali tu vilivyoweza kuruka viunzi vya urasimu huo. Mwanasheria Djidenou Steve Kpoton kutoka mjini Cotonou amesema hatua ya kuvitenga vyama vya upinzani ilitayarishwa kwa makini. Uamuzi huo ni mbaya si kwa Benin tu bali pia kwa nchi zote za jirani.
Baada ya kuondolewa mfumo wa kisoshalisti nchini Benin na kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1990 nchi hiyo ilikuwa imara na mfamo thabiti ya demokrasia. Katiba ya Benin ilikuwa mfano kwa nchi nyingi za Afrika. Mkuu wa asasi ya kiraia "Social Watch” amesema ni vigumu kuffuatilia uchaguzi ambapo ni vyama viwili tu vya serikali vinashiriki vinavyomuunga mkono rais. Amesema wananchi wana haki ya kuwa na uwezekano wa kuchagua baina ya wajumbe wa vyama mbambali la sivyo demokrasia haitakuwa na moyo nchini Benin.
Chanzo: Mwandishi wa DW Gänsler, Katrin (HA Afrika)