1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benin wafanya uchaguzi kukiwa na wasiwasi

11 Aprili 2021

Raia nchini Benin wanapiga kura kwenye uchaguzi wa rais huku hali ikizidi kuwa tete, ambapo wakosoaji wanamtuhumu Rais Patrice Talon kwa kutumia mbinu chafu kuwapiku na kuwatenga viongozi wa upinzani.

Benin |  Anhänger von Präsident Talon
Picha: Katrin Gänsler/DW

Milionea huyo wa biashara ya pamba aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza kuliongoza taifa hilo la Afrika Magharibi mwaka 2016, anakabiliwa na upinzani wa wanasiasa wasio mashuhuri sana, Allassane Soumanou na Corentin Kohoue.

Viongozi wengi wa upinzani wako uhamishoni, wakiwa wameenguliwa kuwania kupitia mageuzi kwenye sheria za uchaguzi au wakiandamwa na uchunguzi wa mahakama maalum.

Benin iliwahi kusifika kama kitovu cha demokrasia kwenye eneo la magharibi mwa Afrika lenye mizozo ya mara kwa mara, lakini hali ya wasiwasi ilitanda kuelekea uchaguzi wa leo, ambapo maandamano yameshuhudiwa kwenye miji kadhaa.

"Upekee wa uchaguzi huu ni kwamba unafanyika katka mazingira ya wasiwasi na machafuko," ilisema taarifa ya asasi moja ya kiraia siku ya Jumamosi (Aprili 10).

Katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Benin, waandamanaji waliweka vizuizi vya barabarani wakizuwiya mamia ya magari kusafiri baina ya pwani na kaskazini.

Mnamo Alkhamis (Aprili 8), watu wawili waliuawa katikati ya mji wa Save, ambako wengine watano walijeruhiwa kwa risasi baada ya wanajeshi kuwarushia waandamanaji mabomu ya machozi na risasi ili kuwatawanya.

"Sifahamu anachokifanya Talon... ikiwa rais huyu ana matatizo na wapinzani, asiwashambulie raia," alisema Philomene M'Betti Tepa, mkaazi wa mji wa kaskazini magharibi wa Boukombe.

Waungaji mkono wa Talon wamekataa shutuma kwamba uchaguzi utachezewa, wakisema mazingira yote ya kura huru na ya haki yapo.

Rais wa Kamisheni ya Uchaguzi, Emmanuel Tiando, aliliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi (Aprili 10) kwamba licha ya kuchelewa shughuli ya kusambaza vifaa vya kura upande wa kaskazini, haimaanishi kwamba hiyo ilikuwa njia ya kuuzuwia uchaguzi usifanyike.

Zaidi ya watu milioni 4.9 wamejiandikisha kupiga kura kwenye vituo 15,531 nchi nzima.

Jumuiya ya kimataifa yataka uchaguzi huru

Bango la Rais Patrice Talon na mgombea wake mwenza, Mariam Talata.Picha: Séraphin Zounyekpe

Ofisi za kibalozi za Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uholanzi pamoja na ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Benin zilizowa wito wa kura kufanyika kwa uhuru na uwazi. 

Kufuatia miaka 17 ya utawala wa kijeshi unaofuata mitazamo ya Marx na Lenin, koloni hilo la zamani la Ufaransa lilifunguwa njia kwa demokrasia ya vyama vingi kuanzia mwaka 1990.

Lakini tangu Talon kuingia madarakani kama mgombea huru, wakosoaji wanasema ameitumia mahakama maalum ya uhalifu wa uchumi na ugaidi na mageuzi ya sheria za uchaguzi kama silaha za kuwaenguwa wagombea wa upinzani.

Bado watu wengi nchini Benin wanakumbuka mgogoro wa kisiasa na ghasia za nchi nzima zilizofuatia uchaguzi wa bunge uliozozaniwa mwaka 2019.

Taifa hilo lililo katikati ya taifa kubwa Nigeria na dogo kabisa la Togo limeshuhudia mafanikio ya kiasi fulani kwenye uchumi wake, ambayo Talon ameyatumilia kama rikodi ya uwezo wake kwenye kampeni. 

"Namuunga mkono rais huyu kwa kuwa tulikuwa na matatizo mengi hapo kabla. Ukosefu wa maji na umeme, lakini sasa afadhali," alisema Ulrich Adjalla, mkaazi wa mji mkuu wa kiuchumi, Cotonou.

"Rais hawezi kuwa mwema kwa kila mtu," alisema kijana wa miaka 28 ambaye hana ajira, lakini "naamini ataunda nafasi za ajira kwa vijana wa nchi hii."

Katika siku za mwisho za kampeni, mji wa Cotonou ulikuwa umejaa mabango ya kampeni kumuunga mkono Talon na mgombea mwenza wake, Mariam Talata.

Kwenye mkutano wake mjini Godomey, Talon alisema alikuwa anarajia ushindi wa moja kwa moja na usiokuwa na haja ya duru ya pili. 

Matokeo yanatazamiwa kutangazwa Jumatatu (Aprili 12) au siku ya pili yake, Jumanne.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW