Benjamin Netanyahu apinga hatua za kuundwa dola la Palestina
17 Novemba 2025
Netanyahu ameyasema hayo wakati Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, likipanga kupigia kura azimio la Marekani kuhusu Gaza, linalotoa nafasi ya mamlaka ya Palestina kupata uhuru wake.
Netanyahu mara zote amekuwa akisisitiza kuwa kuundwa kwa dola la Palestina, ni sawa na kulizawadia kundi la Hamas, akidai hilo litatanua nguvu za kundi hilo na udhibiti wake karibu na mipaka ya Israel.
"Tunapinga kuundwa kwa dola la Palestina. Pingamizi hilo bado lipo litaendelea na bado lina nguvu na halitowahi kubadilika. Nimekuwa nikilipinga hilo kwa miongo kadhaa na nimekuwa nikifanya hivyo ndani na nje ya Israel," alisema Netanyahu.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, linatarajiwa kupigia kura azimio hilo, linalopendekeza uwepo wa kikosi cha kimataifa cha kuleta utulivu Ukanda wa Gaza kinachoratibiwa na Marekani licha ya pingamizi kutoka Urusi, China na baadhi ya mataifa ya kiarabu.
Hamas na makundi mengine ya Palestina yameonya kuhusu azimio hilo la Marekani, wakisema nchi hiyo inataka kuweka mipango katika Ukanda huo, ambayo wanadai yatakuwa yanaipendelea Israel na kuiwanyima wapalestina haki ya kuendesha mambo yao wenyewe.