1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki Kuu ya Ulaya kununuwa dhamana za mabilioni ya euro

22 Januari 2015

Benki Kuu ya Ulaya ECB imekubaliana kuanzisha mpango wa kununuwa dhamana za madeni ya serikali ambapo benki hiyo itachapisha fedha kununuwa euro bilioni 60 za dhamana kuanzia Machi hadi mwishoni mwa Septemba mwakani.

Nembo ya sarafu ya euro ya Benki Kuu ya Ulaya (ECB) mbele ya makao makuu ya umoja huo mjini Frankfurt, Ujerumani.
Nembo ya sarafu ya euro ya Benki Kuu ya Ulaya (ECB) mbele ya makao makuu ya umoja huo mjini Frankfurt, Ujerumani.Picha: Getty Images/A. Dedert

Mpango huo wa Benki Kuu ya Ulaya wa kununuwa dhamana za madeni ya serikali za mabilioni ya euro kwa nia ya kuchangamsha uchumi wa Ulaya.

Kama ilivyokuwa imetarajiwa sana ECB imesema katika taarifa kwamba inaendelea kushikilia kiwango chake kikuu cha kujigharamia kifedha kuwa katika asilimia 0.05 na viwango vyake vyengine viwili vya riba vya kukopesha na kuweka akiba katika asilimia 0.30 na chini ya asilimia 0.20 kila mmoja.

Benki Kuu ya Ulaya ECB inazinduwa mpango huo kwa lengo la kuuchangamsha uchumi unaozorota katika nchi za kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya ambapo kupanda kwa gharama za maisha kumekuja kuwa na taathira mbaya na kuwa katika kiwango cha chini ya asilimia 0.20 ni chini sana ya shabaha ya benki hiyo ya chini ya asilimia mbili.

Ununuzi utafikia euro bilioni 60

Kwa kuzingatia uchambuzi wao wa kawaida wa kiuchumi na kifedha Benki Kuu ya Ulaya imefanya tathmini upya ya kina ya bei za masoko na hatua zilizofikiwa za kuchochea uchumi ambapo baraza la uongozi la benki hiyo likaja na maamuzi hayo ambayo Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi ameyazinduwa jioni hii mjini Frankfurt.

Wakati wa uzinduzi huo Draghi amesema``Imeamuwa kuzinduwa mpango uliotanuliwa wa kununuwa rasilmali wenye kujumuisha mpango wa ununuzi ulioko hivi sasa wa hisa na dhamana.Chini ya mpango huu uliotanuliwa ununuzi wa jumla wa kila mwezi wa sekta za hisa za binafsi na za serikali utafikia euro bilioni sitini.``

Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Frankfurt. (22.01.2015)Picha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Hata hivyo wachumi wanatafautiana iwapo mpango huo wa kununuwa dhamana za madeni ya serikali utaweza kufanyakazi katika kanda hiyo inayotumia sarafu moja ya nchi 19 zikiwa katika hali tafauti za kiuchumi.

Hofu kubwa ilioko Ujerumani ambayo ndio mfadhili mkuu wa Ulaya katika suala la malipo ya fedha ni kwamba hatua hiyo itaziondolea shinikizo serikali kuufanyia mageuzi uchumi wao na kurekebisha taratibu zao za matumizi ya fedha.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri :Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW