Benki ya Dunia na IMF zarejesha uhusiano na Venezuela
17 Aprili 2026
Ndani ya saa chache baada ya tangazo hilo, serikali ya Venezuela nayo ilithibitisha kutambua rasmi uhusiano huo ambao ulikuwa umesitishwa tangu mwaka 2019.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Kristalina Georgieva, amesema nchi wanachama zimeidhinisha kuanza kufanya kazi na serikali ya Venezuela chini ya rais wa mpito Delcy Rodríguez—mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini humo.
Benki ya Dunia nayo ilifuatia kwa kutangaza kurejesha ushirikiano wake na Caracas, uhusiano uliokuwa umesitishwa tangu mwaka 2019.
Akilihutubia taifa, Rais Rodríguez alisema hatua hiyo ni muhimu katika kurejesha haki na nafasi ya Venezuela ndani ya taasisi za kimataifa.
"Tunasawazisha taratibu zote zinazohusu haki na wajibu wa Venezuela ndani ya Shirika la Fedha la Kimataifa. Hii ni hatua muhimu kwa uchumi wa nchi, na pia kwa nafasi yake katika ukanda wetu.", amesema kiongozi huyo.
Kurejea kwa uhusiano huo kutasaidia matatizo ya uchumi wa Venezuela?
Hatua hiyo sasa inafungua uwezekano wa kukusanywa kwa takwimu rasmi za uchumi, utoaji wa ushauri wa kitaalamu na hata msaada wa kifedha endapo Venezuela itawasilisha ombi rasmi.
Uhusiano kati ya pande hizo ulisitishwa mwaka 2019 kufuatia mgogoro wa kisiasa kuhusu uhalali wa uongozi wa nchi hiyo.
Rodríguez, ambaye alikuwa makamu wa rais, alichukua uongozi wa muda mapema mwaka huu baada ya kukamatwa kwa aliyekuwa rais Nicolas Maduro katika operesheni iliyoongozwa na Marekani.
Tangu wakati huo, Washington imekuwa ikiihimiza Caracas kufungua uchumi wake kwa wawekezaji wa kigeni, hasa katika sekta ya nishati.
Wachambuzi wanasema kurejea kwa Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia kunaweza kuimarisha imani ya wawekezaji na kusaidia juhudi za kuufufua uchumi wa Venezuela.
Tangazo hilo limetolewa wakati wa mikutano ya Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia mjini Washington, iliyowakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa uchumi na wawekezaji kutoka kote duniani.
Rodriguez asifu mchango wa Marekani kurejea uhusiano na IMF, Benki ya Dunia
Katika hotuba nyingine, aliishukuru Marekani na washirika wake kwa mchango wao katika kurejesha uhusiano huo.
"Napongeza majadiliano ya kidiplomasia na serikali ya Marekani, na ninamshukuru Rais Donald Trump, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, pamoja na nchi kama Falme za Kiarabu, Brazil na Qatar kwa ushirikiano wao.”
Wakati huohuo, Marekani imeanza kulegeza baadhi ya vikwazo, ikiwa ni pamoja na kuiondolea vikwazo Benki Kuu ya Venezuela.
Hata hivyo, upinzani nchini humo unaendelea kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi mpya wa rais kwa mujibu wa katiba.