1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuwatafuta watu zaendelea Libya na Morocco

14 Septemba 2023

Benki ya Dunia yashirikiana na mamlaka za Morocco na Libya kuandaa ufadhili kwa ajili ya kukabiliana na maafa. Wakati huo huo juhudi za kuwatafuta watu waliokumbwa na maafa zaendelea katika nchi hizo mbili.

Libyen Überschwemmungen
Picha: Esam Omran Al-Fetori/REUTERS

Mkurugenzi wa benki ya dunia ya nchini Uturuki, Humberto Lopez, ameliambia shirika la Habari la Reuters kwamba Libya imeomba msaada wa kimataifa kusaidia katika zoezi la kuwatafuta waliokufa na pia katika juhudi za uokoaji, wakati Morocco imekubali kupokea misaada kutoka kwenye nchi nne huku ikikataa kupokea misaada kutoka kwenye nchi nyingine.

Baadhi ya sehemu za mji wa Derna nchini Libya baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyosababisha maafa.Picha: Esam Omran Al-Fetor/REUTERS

Nchini Libya maalfu ya watu wamezikwa kwenye makaburi ya halaiki katika mji wa Derna, Alhamisi huku wahudumu wakiendelea kupekua kwenye magofu ya nyumba zilizoharibiwa na mafuriko katika mji huo. Meya wa mji huo amesema idadi ya watu waliokufa inaweza kuongezeka hadi mara tatu. Waziri Mkuu wa Libya, Abdulhamid al-Dbeibah, ambaye serikali yake iko mjini Tripoli amesema zaidi ya watu 300 wameokolewa.

Soma:UN: Uharibifu uliosababishwa na mafuriko nchini Libya ungeweza kuzuilika

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema WHO imetoa dola milioni 2 kutoka kwenye mfuko wake wa dharura kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa mafuriko nchini Libya, amesema mahitaji ya kiafya ya walionusurika yanazidi kuongezeka kwa haraka.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus.Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetangaza msaada wa dharura wa dola milioni 10 kwa ajili ya Libya baada ya mafuriko ambayo yamesababisha watu wapatao elfu 20 kufa katika jiji la Derna pekee.

Nchini Morocco waokoaji wameongeza juhudi za kuwatafuta watu katika vijiji vilivyoko milimani vilivyoharibiwa huku matumaini yakizidi kufifia juu ya kuwapata manusura wa tetemeko la ardhi lililotokea wiki iliyopita ambapo karibu watu 3,000 walikufa. watu wengi wameachwa bila makao.

Soma: UNICEF: Watoto takriban 100,000 wameathiriwa na tetemeko la ardhi Morocco

Wakulima katika kijiji kidogo cha Anougal katika jimbo la al-Haous nchini Morocco wanakabiliwa na matatizo makubwa baada ya tetemeko hilo kuharibu mazao yao. Mkulima Mohammed Al Moutawak kutoka eneo hilo amesema mkoa huo umeathiriwa vibaya na tetemeko la ardhi na hasa sekta ya kilimo katika kijiji cha Anougal ambacho kinategemea zaidi kilimo. Ameeleza kwamba kijiji hicho kimeathiriwa kwa kiwango kikubwa na tetemeko hilo kubwa. Hali mbaya ya hewa na ukame wa muda mrefu umekuwa ukiwaathiri wakulima wa nchi za Afrika ya Kaskazini, lakini tetemeko hilo la ardhi limeleta changamoto mpya ambazo zimeanza kujitokeza.

Hali ilivyo nchini Morocco baada ya maafa ya tetemeko la ardhi.Picha: Mosa'ab Elshamy/AP

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa wafadhili kuchangisha kiasi cha dola milioni 71.4 katika miezi mitatu ijayo ili umoja huo uweze kukidhi mahitaji ya watu wapatao 250,000  walioathiriwa na mafuriko nchini Libya.

Vyanzo: RTRE/AFP/DPA/