Bei za bidhaa zimepanda
20 Julai 2015Kufuatia hali hiyo wateja wa benki hizo walionekana katika misururu mirefu katikati ya jiji la Athens ili kushughulikia masuala ya fedha yaliyoahirishwa kwa muda mrefu baada ya kufungwa kwa benki hizo.
Mabenki nchini Ugiriki yalifungwa tangu Juni 29 mnamo wakati serikali ya Ugiriki ikijitahidi kufikia makubaliano na wakopeshaji wa kimataifa na hatua za kudhibiti mitaji zikichukuliwa ili kuepusha kufungwa kwa benki hizo.
Tangu wakati huo wateja wa benki hizo waliweza kutoa kiasi cha pesa kisichozidi dola 65 kwa siku na mihamala mingine ilisimamishwa.
Fedha zaidi zaruhusiwa
Katika kipindi hiki wagiriki wataweza kuchukua fedha hadi euro mia tatu kwa wiki hadi Jumamosi wiki hii wakati ukiandaliwa utaratibu utakaowezesha waweze kutoa fedha katika mabenki hayo hadi kiasi cha dola 420 kwa wiki.
Mabadiliko hayo yanaashiria kwamba wateja sasa hawatalazimika kupanga misururu kila siku katika mabenki bali wanaweza kwenda mara chache ndani ya wiki katika taasisi hizo na kuchukua kiasi kikubwa cha fedha.
Aidha hatua hiyo imefungua pia njia ya wateja kuanza tena kufanya mihamala ya kutuma fedha kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya taifa hilo.
Watu waliweza kufanya mihamala ya kusafirisha fedha kwa kulipia bili za umeme na maji na mfanyakazi mmoja wa benki moja nchini humo aliliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa ya kuwa wengi wao walikuwa ni wafanyabiashara wadogo na wakati walioweza kufanya mihamala hiyo kwa ajili ya malipo.
Amri ya kutofanya mihamala kwa kutuma fedha nje ya nchi itaendelea kutekelezwa isipokuwa tu kwa ajili ya kulipia ada kwa wanafunzi wanaosoma ng'ambo na malipo kwa ajili ya wale wanaopata huduma ya matibabu nje ya nchi.
Hata hivyo wagiriki sasa wataweza kutumia tena kadi zao za benki kufanya mihamala ya kimataifa kwa ajili ya malipo ya bidhaa au huduma wanazohitaji pasipo kulipa pesa tasilimu kulingana na kiwango kitakachoamriwa na kila benki nchini humo.
Bei za bidhaa zimepanda
Hatua ya kufungwa kwa mabenki nchini Ugiriki hapo kabla kunakadiriwa kuisababishia hasara ya fedha yenye thamani ya sarafu ya euro kiasi cha bilioni tatu.
Serikali ya Ugiriki baada ya ubishi wa muda mrefu hatimaye ilikubali mashariti magumu iliyopewa na mataifa washirika wenzake katika umoja wa sarafu ya euro ili iweze kupata fedha za kujikwamua na hali ya ukata kwa kufanya marekebisho katika mifumo yake ya pensheni pamoja na kupandisha viwango vya kodi ikiwa ni pamoja na kukubaliana na sera ya ubinafisishaji mambo ambayo iliyakataa hapo kabla.
Hatua hiyo imesabaisha kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali kuanzia leo kama vile sukari na kakao kutoka asilimia 13 hadi asilimia 23.
Kwa upande mwingine kodi kwa madawa, vitabu na magazeti imeshuka kutoka asilimia 6.5 hadi asilimia 6.0.
Mwandishi: Isaac Gamba/ DPAE/AFPE
Mhariri:Josephat Charo