1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naftali Bennet akutana na Mohammed bin Zayed Al Nahyan

13 Desemba 2021

Waziri mkuu wa Israeli Naftali Bennet, amekutana kwa mazungumzo na mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan kama sehemu ya ziara yake rasmi katika Umoja wa Falme za Kiarabu UAE

Vereinigte Arabische Emirate Abu Dhabi | Naftali Bennett und Abdullah Bin Zayed
Picha: Haim Zach/Israel Gpo/ZUMA Wire/imago images

Ofisi ya Benett imesema  mkutano huo wa ana kwa ana kati ya viongozi hao wawili ulikamilika baada ya muda wa zaidi ya masaa mawili. Ofisi hiyo imeongeza kwamba baadhi ya masuala yalioangaziwa ni pamoja na biashara na mazingira, lakini ni maelezo machache yaliotolewa huku Iran na Palestina zikikosa kutajwa moja kwa moja.

Israeli na UAE zaonesha ari ya kuimarisha ushirikiano

Ofisi hiyo imeendelea kusema kuwa pande zote mbili ziliangazia ari ya kuimarisha ushirikiano kati yao na hatua za pamoja katika jitihada za kuimarisha maslahi ya pande zote pamoja na kuchangia katika kudumisha utulivu, usalama na maendeleo katika kanda hiyo. Msemaji wa Bennet ameliambia shirika la habari la WAM katika Umoja huo wa Falme za Kiarabu kwamba ziara hiyo ilionesha ukweli mpya kwa Mashariki ya Kati na kwa mtazamo wake, huu ndio ukweli mpya ambao kanda hiyo inashuhudia akisema wanashirikiana kuhakikisha maisha bora ya siku zijazo kwa watoto wao.

Naftali Bennet apokelewa kwa gwaride la kijeshi la Umoja wa Falme za KiarabuPicha: Haim Zach/Israel Gpo/ZUMA Wire/imago images

Waziri huyo mkuu wa Israel pia atakutana na mawaziri wa teknolojia na utamaduni wa UAE wakati wa ziara yake na alizungumzia kuhusu fursa zisizo na kikomo za baadaye za kuendeleza biashara. Aliongeza kuwa Israeli kama UAE ni kitovu cha kikanda cha biashara na kwamba ushirikiano wao unatoa fursa za kiuchumi ambazo hazijawahi kushuhudiwa sio tu kwa mataifa hayo mawili lakini kwa mataifa zaidi.

Ziara hiyo ya Naftali inafanyika wakati serikali yake ikirejesha upya shinikizo dhidi ya kuanza tena kwa mazungumzo ya kimataifa ya kuufufua Mkataba wa Mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu dunian juu ya mpango wake wa nyuklia, ambao Iran inasisitiza kwamba ni kwa ajili ya matumizi salama. Mazungumzo hayo mjini Vienna yanadhamiria kuirejesha Marekani iliyoondolewa na utawala wa Trump mwaka 2018 kwenye mkataba huo na pia kuifanya Iran kuheshimu kikamilifu ahadi zake. Hata hivyo, Bennett anataka mazungumzo hayo yasitishwe, akiituhumu Iran kwa kile anachokiita "ghiliba ya nyuklia" na kwamba itatumia mapato yanayotokana na kuondolewa vikwazo kuimarisha silaha zake zitakazoidhuru Israel.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW