Bennett kukutana na mfalme, mrithi wa ufalme wa Bahrain
15 Februari 2022Baada ya kuwasili siku ya Jumatatu (Februari 14) na kulakiwa kwa hamasa kubwa mjini Manama na Waziri Mambo ya Nje wa Bahrain, Abdullatif bin Rashid Al-Zayani, hivi leo (Jumanne, Februari 15), Bennett anatazamiwa kukutana na Mfalme Hamad na pia mrithi wa kiti cha ufalme aliye pia waziri mkuu wa taifa hilo dogo, Salman bin Hamad.
Ziara hii ya Bennett ni ya sehemu ya jitihada za hivi karibuni kabisa kujikurubisha na mataifa ya Kiarabu, kufuatia kile kinachoitwa Mkataba wa Abraham uliosimamiwa na Marekani mwaka 2020, ambao unavunja makubaliano ya muda mrefu ya mataifa ya Kiarabu kutokuwa na mahusiano na Israel bila ya kwanza kuwepo kwa suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa Israel na Palestina.
Bahrain na mshirika wake wa karibu, Umoja wa Falme za Kiarabu, zilizifuata Misri na Jordan kwenye kuanzisha mafungamano na Israel baada ya kusaini makubaliano yaliyosimamiwa na rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump. Bennett aliutembelea Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Disemba mwaka jana.
Mkataba wa ulinzi kati ya Israel na Bahrain
Kabla ya kuondoka kuelekea Bahrani hapo jana, Bennet alisema: "Kwenye nyakati za majaribu kama hizi, ni muhimu kwamba tunatuma ujumbe wa nia njema kutoka ukanda huu, ujumbe wa ushirikiano wa kusimama pamoja dhidi ya changamoto za pamoja."
Ziara ya Bennett inafuatia ile ya waziri wake wa ulinzi, Benny Gantz, ambaye aliwasili mjini Manama mapema mwezi huu na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ulinzi kati ya nchi hizo mbili.
Mkataba huo unahusisha masuala ya ujasusi, ununuzi wa silaha na mafunzo ya pamoja, ambapo Gantz alisema ungeimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia kati ya Israel na Bahrain.
Mkataba wa Nyuklia wa Iran
Ziara hii pia inakuja katika wakati ambapo wasiwasi kwenye ukanda wa Ghuba na Mashariki ya Kati umeongezeka juu ya mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Jamhuri hiyo ya Kiislamu imo kwenye mchakato wa majadiliano ya moja kwa moja na Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani na Urusi, huku mazungumzo yake na Marekani yakiwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja mjini Vienna, Austria.
Lengo la mazungumzo hayo ni kuufufua Mkataba wa Nyuklia wa mwaka 2015 uliopewa jina la JCPOA, ambao uliipa Tehran akhuweni ya vikwazo dhidi yake kwa masharti ya taifa hilo kudhibitiwa mpango wake wa nyuklia.
Hata hivyo, Marekani ilijiondowa kwenye mkataba huo mnamo mwaka 2018 chini ya utawala wa Trump, hali iliyotishia kurejea upya kwa mkwamo wa kimataifa juu ya Iran.
Juhudi za kuurejesha upya zilizoanza mwezi Novemba mwaka jana zinapingwa na Bennet, anayedai kuwa hatua yoyote ya kuiondolea vikwazo Iran ni kulipa taifa hilo hasimu uwezo wa kujijenga kisilaha dhidi ya Israel.