Benzema awasha moto Bernabeu, awatimua PSG
10 Machi 2022Kuna wakati ambapo Karim Benzema alizomewa na mashabiki wa Real Madrid kwa kutodhihirisha kipaji chake chote, kwa kutofumania nyavu vya kutosha, kwa kutojitokeza katika mechi kubwa. Hata ingawa alikuwa amewanyamazisha wakosoaji wake katika miezi ya karibuni, hakuna anayeweza tena kumtilia mashaka mshambuliaji huyo wa Ufaransa baada ya kuongeza jina lake katika historia ndefu ya klabu hiyo kwenye Champions League.
Benzema alifunga mabao matatu katika dakika 18 pekee Jumatano usiku na kuiondoa Paris Saint-Germain iliyopigwa na bumbuwazi na kuiweka klabu hiyo ya Uhispania katika kinyang'anyiro cha kushinda taji la Ulaya na la Ligi ya Uhispania.
Kwa mechi moja na nusu, Kylian Mbappe alikuwa anaiongoza PSG kuelekea ushindi mnono kwa kufunga mabao mawili mazuri kabisa yaliyoonyesha ni kwa nini mahasimu wengi wanammezea mate nyota huyo wakimtaka ajiunge nao msimu ujao.
Hiyo ni hadi Benzema alipoiongoza Madrid kwa vita vikali vya kutokea nyuma katika kipindi cha pili na kupata ushindi wa jumla ya mabao 3-2 katika mikondo miwili.
Katika mechi nyingine iliyochezwa Jumatano usiku, Manchester City ilitoka sare tasa na Sporting Lisbon uwanjani Etihad na hivyo kutinga robo fainali kwa jumla ya mabao 5-0.
City tayari walikuwa wamefanya kazi ngumu katika mechi ya mkondo wa kwanza nchini Ureno wiki tatu zilizopita mjini Lisbon. Na ndio maana kocha Pep Guardiola aliwaweka uwanjani vijana wasiokuwa na uzoefu sana.
AFP, DPA, AP