BERLIN : Chama cha CDU chatishia kuvunja mazungumzo na SPD
5 Oktoba 2005Chama cha kihafidhina cha Christian Demokrat CDU nchini Ujerumani hapo jana kimetishia kuvunja mazungumzo na chama cha Social Demokrat SPD juu ya kuunda serikali ya mseto iwapo chama hicho hakitoachana na dai lake la kutaka Gerhard Schroeder aendelee kuwa Kansela.
Chama cha CDU cha Angela Merkel ni chama kikubwa bungeni kwa kuwa na wingi wa viti vinne zaidi kufuatia uchaguzi mkuu ulioshindwa kutowa mshindi dhahiri wiki mbili zilizopita. Afisa mmoja wa CDU amekaririwa akisema kwamba mazungumzo kati ya chama chake na SPD yaliopangwa kufanyika leo mchana yatasitishwa iwapo chama hicho cha SPD hakitochukuwa hatua juu ya suala hilo.
Hapo Jumaatatu Schroeder alidokeza kwamba yuko tayari kuachana na dai lake la kubakia kuwa Kansela ili asiwe kikwazo cha kuundwa serikali imara ya muungano mkuu kati ya vyama hivyo viwili vikuu vya kisiasa.
Hata hivyo uongozi kwenye chama chake cha SPD unasisitiza aendelee kubakia kuwa Kansela kwa kipindi cha tatu.