Berlin. China imeikasirikia Ujerumani kutokana na kansela kukutana na Dalai Lama.
29 Septemba 2007Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani amesema kuwa China bado imechukizwa kuhusiana na mkutano baina ya kansela wa Ujerumani na Dalai lama wiki iliyopita. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema kuwa mazungumzo na waziri wa mambo ya kigeni wa China Yang Jiechi siku ya Ijumaa yaligusia kuhusu Iran na Myanmar lakini mkutano uliofanyika siku ya Jumapili kati ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel na kiongozi wa dini ya Kibudha katika jimbo la Tibet anayeishi uhamishoni uliofanyika mjini Berlin umejitokeza kuwa suala kuu. China imekasirishwa na mkutano huo , ikiionya Ujerumani kuwa mahusiano baina ya nchi hizo mbili yameathirika na kusisitiza kuwa Dalai Lama ni mtu hatari ambaye anataka uhuru wa jimbo la Tibet. China kwa kawaida inashutumu ziara za Dalai Lama nje ya nchi , ambaye alikimbia Tibet na kwenda kuishi India mwaka 1959 wakati wa vuguvugu la uamsho lililoshindwa dhidi ya utawala wa China.