Berlin. Kansela Schroeder awahakikishia Wajerumani kupata kazi kwa kukataa shinikizo la umoja wa Ulaya kulegeza masharti ya sekta ya huduma.
10 Aprili 2005Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder ameishambulia tume ya umoja wa Ulaya jana , akisema Ujerumani haitaongeza malipo yake kwa bajeti ya umoja huo na amekataa mipango ya kufungua milango katika sekta ya huduma.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi katika jimbo la North Rhine-Westphalia, Bwana Schroeder ameongeza uzito katika mapambano ya muda mrefu sasa na utawala wa jumuiya ya Ulaya kuhusiana na pendekezo la bajeti ya jumuiya hiyo katika miaka ya 2007 hadi 2013.
Akizungumzia hadi inayozidi kuwa ya wasi wasi nchini Ujerumani kutokana na uwezekano wa wafanyakazi kutoka mataifa ya mashariki ya Ulaya kwa kuchukua kazi za Wajerumani kwa kulipwa ujira mdogo, na masharti duni, Bwana Schroeder pia amesisitiza kuwapo na uhakika wa kazi kabla ya kukubali mipango ya kulegeza masharti ya sekta ya huduma kama inavyotakiwa na jumuiya ya Ulaya.