BERLIN : Kumbukumbu ya Miaka 46 ya Ukuta wa Berlin
14 Agosti 2007Kumbukumbu za miaka 46 ya kuanza kwa ujenzi wa Ukuta wa Berlin zimetiwa kiwingu na usahidi mpya wa amri za kuwaua watu wanaojaribu kuikimbia iliokuwa Ujerumani ya Mashariki hapo zamani.
Meya wa jiji la Berlin Klaus Woworeit ameweka shada la mauwa hapo jana kwenye eneo la kumbukumbu katika mtaa wa Bernauer mtaa ambao ulikuwa ndio unakopitia mpaka kati ya mji wa Berlin uliogawika.
Hata hivyo kumbukumbu hiyo ilifanyika chini ya utata mpya juu ya kugundulikana wiki iliopita kwa waraka wa mwaka 1973 ambao uliwataka walinzi wawauwe kwa kuwapiga risasi watu wanaotaka kutoroka Ujerumani ya Mashariki na kukimbilia Ujerumani ya Magharibi wakiwemo wanawake na watoto.
Viongozi wa zamani wa Ujerumani Mashariki wanaendelea kukanusha kwamba kulikwepo na amri hizo.
Wakati wa kuwepo kwa ukuta huo kwa miaka 26 watu takriban 133 wameuwawa wakati wakijaribu kutoroka kutoka Ujerumani ya Mashariki.