BERLIN: Kundi la Islamic Jihad ladai kuhusika na njama ya mashambulio ya kigaidi
12 Septemba 2007Wizara wa mambo ya ndani ya Ujerumani imesema kundi la kigaidi la Islamic Jihad limetangaza kuhusika na njama ya wiki iliyopita ya kutaka kufanya mashambulio ya kigaidi.
Maeneo yaliyolengwa katika njama hiyo ni uwanja wa ndege wa Frankfurt, kambi ya jeshi la Marekani ya Ramstein na balozi za Marekani na Uzbekistan hapa Ujerumani.
Katika taarifa yake wizara ya mambo ya ndani imesema wataalmu wa komputya wa serikali wamelitathimini tangazo la kundi la Islamic Jihad kwenye mtandao wa internet kuwa la kweli.
Watu watatu walikamatwa mnamo tarehe nne mwezi huu kwa kushukiwa kupanga mashambulio makubwa ya kigaidi.
Mashambulio hayo yalilenga kuishinikiza Ujerumani iifunge kambi ya jeshi lake la anga ya Termez nchini Uzbekistan.
Kambi hiyo iliyo katika mpaka wa Uzbekistan na Afghanistan hutumika kutoa msaada wa uratibu kwa wanajeshi 3,000 wa Ujerumani wanaohudumu katika kikosi cha kimataifa nchini Afghanitan.