1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin: maelfu waunga mkono na kupinga maandamano ya AfD

Yusra Buwayhid
27 Mei 2018

Wafuasi 5,000 wa  chama mbadala kwa Ujerumani (AfD) wameandamana mjini Berlin Jumapili, lakini idadi hiyo ilikuwa ndogo ikilinganishwa na walioandama kuipinga AfD.

Berlin AfD-Demonstration
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Maelfu ya watu wameandamana Jumapili katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin. Ni maandamano yanayohusisha pande mbili tofauti. Upande wa wafuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani AfD, kinachopinga uhamiaji pamoja na Uislamu. Na waandamanaji wanaoipinga AfD wakitumia kauli mbiu ya "Wacha chuki.”

Maafisa zaidi wa polisi walishika doria kutenganisha pande hizo mbili za waandamanaji ili kuepusha vurugu.

Katika ukurasa wao wa Twitter, idara ya polisi imesema wametumia kemikali ya pilipili ya kutoa machozi kuwazuia waandamanaji wasivunje mpaka uliowekwa kuwatenganisha.

Beatrix von Storch, mwanachama muhimu wa AfD, amewaambia wafuasi wapatao 2,000 waliokusanyika katika maandamano hayo kwamba mchezaji soka wa timu ya taifa ya Ujerumani Mesut Ozil licha ya kuwa na uraia wa Ujerumani sio Mjerumani. Mchezaji soka huyo, mwenye asili ya Kituruki, amekosolewa vikali hivi karibuni kwa kukutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

AfD inaipinga serikali ya Kansela Angela Merkel kwa kuruhusu idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi kuingia Ujerumani. Kama ilivyo katika maandamano ya nyuma ya AfD ya kupinga Uislam nchini Ujerumani, kulikuwapo na watu waliokuwa wakipiga mayowe "Merkel lazima aondoke," wakimaanisha kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Maandamano hayo ya AfD ni ya kwanza kuonesha umma nguvu yao tangu ilipoingia bungeni kwa mara ya kwanza na kuwa chama kikuu cha upinzani.

Maandamano dhidi ya AfD, BerlinPicha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

AfD: baadhi ya wafuasi waogopa kujitokeza

Wanaotarajiwa kuhutubia katika maandamanohayo ni viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho, ikiwa ni pamojana Joerg Meuthen and Alexander Gauland.

Viongozi hao wana kawaida ya kupinga uamuzi wa Kansela Merkel wa kuruhusu idadi kubwa ya wahamiaji kuingia nchini Ujerumani wengi wao wakiwa Waislam, wakati wa kilele wa mgogoro wa wahamiaji barani Ulaya mwaka 2015.

"Merkel amesababisha taharuki kubwa," amesema mwanachama wa AfD, Christine Moessl mwenye umri wa miaka 41. "Na sasa tunajua kwamba Waislam wengi wenye misimamo mikali walikuwa miongoni mwa wakimbizi, na hawaheshimu wanawake. Tunahitaji kujihisi tuko salama," ameongeza Moessl.

Baada ya awali kutabiri wafuasi 10,000 wa AfD watajitokeza, waandaaji baadaye walisema watafurahi hata wakijitokeza 5,000.

Mkuu wa AfD mjini Berlin, Georg Pazderski alisema kabla ya maandamano kwamba wengi bado wanaogopa kujidhihirisha kuwa ni wafuasi wa AfD. Hata baada ya chama hicho kuchukua asilimia 13 ya kura, na kushinda viti vyao vya kwanza katika bunge la kitaifa wakati wa uchaguzi wa mwaka jana.

Lakini pia kulikuwa na watu wapatao 20,000 walioandamana kuyapinga maandamano hayo ya AfD - kulingana na makadirio ya polisi - wengi wao wakiwa vijana, jambo linaloashiria mgawanyiko unaoshuhudiwa nchini Ujerumani tokea mgogoro wa wahamiaji wa mwaka 2015.

Maandamano hayo ya Jumapili yalikuwa ni ya amani. Mtu mmoja tu ameripotiwa kupata jeraha dogo, huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afp/dpa

Mhariri: John Juma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW