BERLIN : Merkel ataka nchi tajiri kutimiza ahadi kwa Afrika
25 Aprili 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye nchi yake inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya amesema hapo jana atazishinikiza nchi tajiri kutimiza ahadi zao za misaada kwa Afrika wakati Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair amesisitiza kwamba Ulaya yenyewe itaathirika iwapo haitochukuwa hatua ya kutatuwa matatizo ya Afrika.
Viongozi hao wawili walikuwa na mazungumzo mjini Berlin na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ambaye hivi sasa ni mwenyekiti wa Jopo la Maendeleo la Afrika lenye kufuatilia maendeleo ya nchi tafauti za Afrika katika kulisaidia bara hilo.
Merkel amesema pande zote mbili nchi wafadhili na zile zenye kupokea misaada zinatakiwa kutimiza ahadi ilizotowa katika mkutano wa viongozi wa Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo ya Viwanda Duniani uliofanyika huko Gleaneagles nchini Uingereza hapo mwaka 2005 ambapo Blair alilifanya suala la kupiga vita umkaskini barani Afrika kuwa lengo muhimu.
Katika mkutano huo Kundi la Mtaifa Manae lilikubali kuongeza msaada wake kufikia dola bilioni 50 na nchi za Umoja wa Ulaya zikaahidi kuongeza michango yake ya misaada kwa asilimia 0.5 ya pato la jumla la taifa ifikapo mwaka 2010.
Merkel ameiweka Afrika juu kwenye agenda katika mkutano wa viongozi wa Kundi la Mataifa Manane lenye maendeleo makubwa ya viwanda utakaofanyika wakati Ujerumani ikishikilia urais wa kundi hilo katika mji wa Heilegendamm hapo tarehe 6 hadi tarehe 8 mwezi wa Juni.
Nchi kadhaa za Afrika zimealikwa kuhudhuria mkutano huo.