Berlin :Mpango wa waziri wa ndani Schäuble wakosolewa
16 Julai 2007Waziri wa ndani wa Ujerumani Wolfgang Schäuble anajaribu kupunguza mvutano katika serikali kuu ya mseto ya Shirikisho, uliosababishwa na mapendekezo yake ya karibuni kuhusu vita dhidi ya ugaidi. Mtaalamu wa maswala ya ndani wa chama cha Social Democrats SPD mshirika katika serikali kuu ya muungano Bw Dieter Wiefelspütz, aliliambia gazeti la kila siku Frankfurter Rundschau, kwamba Bw Schäuble amekua ni mzigo katika muungano huo.
Waziri huyo wa ndani kutoka chama cha Christian Democratic Union-CDU, amesema matamshi yake katika mahojiano juu ya kuwalenga na kuwauwa washukiwa wa ugaidi yalifahamika vibaya. Katika hatua isiyo ya kawaida, rais wa Ujerumani Horst Köhler alimkosoa hadharani Bw Schäuble mwishoni mwa juma lililopita, kwa mapendekezo yake juu ya kupambana na ugaidi.