1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN. Schroeder apendekeza uchaguzi mkuu wa mapema.

23 Mei 2005

Chama cha upinzani hapa nchini Ujerumani, Chistian Democrats, CDU, kiliibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika katika mkoa wa viwanda wa North Rhine-Westphalia.

Katika hatua yake ya kwanza baada ya chama chake cha SPD kushindwa vibaya katika jimbo hilo ambalo limekuwa likilimiliki kwa muda wa miaka 39, kansela Gerhard Schroeder amependekeza uchaguzi mkuu ufanyike mapema, badala ya kusubiri hadi mwezi Septemba mwaka ujao.

Kushindwa kwa chama cha SPD katika mkoa huo kunaendeleza kushindwa kwake katika maeneo mengine humu nchini. Mwaka wa 1999 chama hicho kilitamba katika majimbo 11 kati ya majimbo yote 16, lakini sasa kimejipatia ushindi katika majimbo matano pekee.

Matokeo ya mwanzo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi yalionyesha kwamba chama cha CDU kilijinyakulia asilimia 45 ya kura huku chama cha SPD kikifuata nyuma kwa asilimia 37.2. Chama cha Kijani kilipata asilimia 6.1 huku chama cha Free Democrats kikiwa na asilimia 6.3.

Schroeder amesema kushindwa kwa chama chake kunatilia shaka sera yake ya maongozi na ikiwa kweli chama hicho kinatakiwa kuendelea kulitawala taifa hili wakati ambapo Ujerumani inafanya mageuzi muhimu katika sekta mbalimbali.

Kiongozi wa chama cha CDU, Angela Merkel, ambaye huenda apambane na kansela Schroeder kwenye kinyang´anyiro kijacho, katika juhudi zake za kuwa kansela wa kwanza mwanamke hapa Ujerumani, amesema wapiga kura wamekiamini chama hicho wakikitaka kuunda sera itakayopunguza ukosefu wa ajira hapa nchini. Ameliunga mkono pendekezo la Schroeder la uchaguzi wa mapema akisema Ujerumani litakuwa taifa bora zaidi pasipo muungano wa chama cha SPD na cha Kijani.

Kwa mujibu wa katiba ya Ujerumani uchaguzi unaweza kufanyika mapema iwapo rais atauitisha. Serikali pia lazima ishindwe katika kura ya kutokuwa na imani nayo bungeni.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW