BERLIN : Schroeder bado ana tamaa ya kushinda uchaguzi
11 Septemba 2005Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani amesema leo hii wimbi la ushindi linageuka upande wake ikiwa imebakia wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu ambapo imedokezwa kuwa atashindwa na mpinzani wake wa kihifadhina Angela Merkel.
Schroeder alikuwa akizungumza baada ya uchunguzi wa maoni kuonyesha kwamba pengo liliopo baina ya vyama vyao linazidi kupunguwa na kufikia pointi saba lakini wachunguzi wa mambo wanasema tafuati hiyo imebakia kuwa kubwa kuweza kuiziba hata kwa kansela huyo mwenye kipaji ambaye katika uchaguzi uliopita mwa mwaka 2002 alikuwa nyuma lakini akashinda.
Schroeder amekaririwa akiliambia gazeti la Bild la toleo la Jumapili kwamba kila anapokwenda hulakiwa na uungaji mkono mkubwa wa watu na kwamba wimbi linabadilika.
Mpinzani wake Bibi.Merkel matamshi yake kwa gazeti jilo leo yalikuwa ya tahadhari zaidi ambapo amesema kampeni ya uchaguzi inafungwa tu siku ya uchaguzi wenyewe tarehe 18 Septemba na kwamba wana kila nafasi ya kushinda uchaguzi huo na kuunda serikali ya mseto na chama cha Free Demokrat ambacho kinafanya mkutano wake wa mwisho mkuu mjini Berlin kabla ya uchaguzi huo wa taifa wiki ijayo.
Viongozi wa chama hicho wametowa wito wa kuregezwa kwa taratibu kwenye soko la ajira ndani ya nchi ili kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira.