BERLIN : Ujerumani kuendelea kuijenga Afghanistan
20 Mei 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani hapo jana ameahihdi kuendelea na juhudi za kuijenga upya Afghanistan baada ya shambulio la kujitolea muhanga maisha kuuwa wanajeshi watatu wa Ujerumani na kujeruhi wengine wawili kwenye soko katika mji wa Kunduz.
Merkel amesema katika taarifa kwamba jeshi la Ujerumani linatekeleza shughuli muhimu kwa ajili ya kuijenga upya Afghanistan na kuleta utulivu nchini humo na kwamba lengo la washambuliaji hao ni kuharibu mafanikio yaliofikiwa katika mchakato wa ujenzi mpya wa nchi hiyo.
Waasi wa kundi la Taliban wamedai kuhusika na shambulio hilo kaskazini mwa Afghanistan ambapo kwa kawaida ni eneo tulivu. Shambulio hilo ni baya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea mwaka 2003 kwa wanajeshi 3,000 wa Ujerumani ambao wameambatanishwa na Kikosi cha Usaidizi wa Usalama cha Kimataifa ISAF kilioko chini ya usimamizi wa kikosi cha Umoja wa Kujihami wa Mataifa Magharibi NATO.
Mripuko huo pia umeuwa raia sita wa Afhanistan na kujeruhiwa wengine 13 pamoja na mkalimani wa wanajeshi wa Ujerumani.