BERLIN: Wanajeshi wawili wa Ujerumani wasimamishwa kazi
27 Oktoba 2006Jeshi la Ujerumani limewasimamisha kazi maafisa wake wawili kuhusiana na kashfa ya wanajeshi waliopiga picha na mafuvu ya vichwa vya binadamu nchini Afghanistan.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Berlin, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, amesema wanajeshi wengine watatu wanachunguzwa kufuatia picha mpya zilizoonyeshwa na runinga ya RTL hapo jana, ambazo inasemekana zilipigwa mnamo mwaka wa 2004.
Waziri Jung amesema tabia hiyo haina nafasi katika jeshi la Ujerumani.
´Ninataka tena kusisitiza wazi kwamba matamshi yangu kuwa afisa yeyote mwenye tabia kama hiyo anaenda kinyume na mafunzo yetu na utawala wa ndani. Ndio maana hana nafasi katika jeshi la Ujerumani, Bundeswehr. Kuanzia sasa tumewasimamisha kazi maofisa hao wawili wa jeshi.´
Waziri Jung amesema afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Ujerumani, atasafiri kwenda Afghanistan kuchunguza motisha na tabia ya wanajeshi walio nchini humo.
Katika mahojiano yake na gazeti la Bild, lilichochapisha picha za kwanza za wanajeshi Jumatano iliyopita, mmoja wa wanajeshi waliohusika amesema kisa hicho kilifanyika karibu na mji mkuu wa Afghanstan, Kabul mwaka wa 2003.
Aidha amesema tabia hiyo ilisababishwa na hofu dhidi ya mashambulio ya waasi miongoni mwa wanajeshi.
Wakati haya yakiarifiwa, kijana aliyewashambulia watu kwa kisu mjini Berlin miezi mitano iliyopita, ameshtakiwa kwa makosa ya kukusudia kuua. Kijana huyo amekuwa akizuilia na polisi tangu alipokamatwa.