BERLIN.Mawaziri wa mambo ya nje waazimia kufufua mazungumzo ya umoja wa ulaya
25 Oktoba 2006Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mwenziwe wa Uingereza bibi Margaret Beckett wana azimia kufufua mazungumzo ya katiba ya umoja wa ulaya.
Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Ujerumani na Uingereza waliyasema hayo baada kukutana mjini Berlin. Viongozi hao pia wametangaza mipango ya jitihada za kuitaka Uturuki itambue taifa huru la Cyprus ya Ugiriki kufikia mwisho wa mwaka huu.
Hatua ya Uturuki ya kukataa kulitambua taifa hilo lililo katika mgawanyiko wa visiwa vya Mediterranean chini ya utawala wa Ugiriki ni kikwazo kinacho izuia Uturuki kujiunga na nchi za umoja wa Ulaya.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapendelea Uturuki iwe na uhusiano wa kiwango fulani tu na umoja wa ulaya badala ya kuwa mwanachama kamili wa umoja huo. Ujerumani inatarajiwa kuchukuwa uenyekiti wa umoja wa ulaya unaozunguka katikati ya mwaka 2007.
Wakati huo huo rais wa Shirikisho la Jamuhuri ya Ujeumani Horst Köhler amekana kutia saini mswaada wa sheria uliopendekezwa na serikali ya kansela Angela Merkel juu ya kubinafsishwa shughuli za usimamizi wa anga.
Msemaji wa rais ameeleza kuwa baada ya kuutathmini kwa kina mswaada huo rais Köhler amesema utakiuka katiba ya nchi. serikali ya mseto ya kansela Angela Merkel ilitaka mabadiliko hayo ili kuzalisha mapato kufikia Eruo bilioni moja.