1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki imeshuka

Veronica Natalis
30 Septemba 2021

Baraza la  biashara la Afrika Mashariki limesema kuwa biashara ya ndani ya jumuiya hiyo iliporomoka kwa asilimia 5.5 mnamo mwaka 2020, kutokana na janga la virusi vya Corona.

Uganda | Coronavirus | Straßenhändler
Picha: Hajarah Nalwadda/Xinhua/picture alliance

Katika kikao maalumu cha kujadili biashara na uwekezaji baada ya janga la Covid- 19, mkurugenzi wa baraza hilo amesema, sekta binafsi ni kiungo muhimu katika mkakati wa kufufua uchumi ndani ya jumuiya hiyo. 

Kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao pamoja na mambo mengine kimebainisha kuwa, biashara ndani ya nchi zote sita za jumuiya ya Afrika Mashariki ilipungua kwa asilimia 5.5 mnamo mwaka 2020 hadi dola za Kimarekani bilioni 5.9 huku bidhaa zinazotumwa katika mataifa ya nje zilifikia kiwango cha bilioni 16.2 kwa mwaka 2020, ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu ikilinganishwa na mwaka 2019.

Mkurugenzi mkuu wa baraza la biashara la Afrika Mashariki JBosco Kalisa wakati akifungua kikao hicho, alibainisha kuwa sekta binafsi zina nafasi kubwa ya kufufua uchumi wa jumuiya hiyo kongwe barani Afrika.

Biashara ya maua ni maarufu huko KenyaPicha: Getty Images/AFP/P. Meinhardt

"Malengo ya mkutano huu pia ni kujadili kwa upana, kupeana mawazo ni jinsi gani baraza la biashara la Afrika Mashariki wanaweza kushirikiana na wadau wa maendeleo kama serikali za nchi zote sita ni kuona ni kwa namna gani wanaweza kusukuma mbele ajenda ya kufufua tena uchumi.  Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na baraza la biashara la Afrika Mashariki zinamkakati mpya wa kufanikisha jambo hilo.”

Kikao hicho pia kilifafanua kuwa baraza la biashara la Afrika mashariki, kwa kushirikiana na kampuni ya utafiti wa kiuchumi na wakfu wa Bill na Melinda, walifanya utafiti kuhusu athari za janga la Covid-19, ambao utasaidia kutoa mwelekeo wa kuweka sera ambazo zitakuwa chachu ya kufufua uchumi katika sekta za viwanda, utalii, kilimo, usalama wa chakula pamoja na sekta ya usafirishaji ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki. Alhaji Rashid Kiboa ni mkurugenzi wa biashara kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Wakati wa kuandaa mpango wa jumuiya ya Afrika Mashariki wa kufufua uchumi, tuliangalia vitu vingi akiwapo kuangalia nini kinahitajika kwa nchi husika ili kufanikiwa mpango huo. Kuna malengo kama matatu ambayo tumeyaweka ikiwapo   mipango ya nchi moja moja kwanza  ya nini kinatakiwa kufanyika baada ya Corona.”

Kulingana na umoja wa Mataifa, nchi za Afrika zinaweza kujijenga upya kiuchumi kwa kuongeza kasi ya ukuaji wa viwanda vya Afrika, na kuimarisha uchumi wake kupitia sekta binafsi.