1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara ya maziwa ya wanawake wa Nandi nchini Kenya

30 Aprili 2025

Mafunzo ya usimamizi wa ngombe na kilimo cha nyasi za kisasa zinazoimarisha afya ya mifugo vimewabadilishia maisha. Mpango huo unadhamiria kuimarisha miradi ya kilimo na mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.

Mtaalam akikagua maziwa yaliyowasilishwa ili kuhakikisha yako salama kwa matumizi ya binadamu
Mtaalam akikagua maziwa yaliyowasilishwa ili kuhakikisha yako salama kwa matumizi ya binadamuPicha: Thelma Mwadzaya/DW

Wanawake wa eneo la Nandi wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kuja pamoja na kuimarisha biashara yao ya maziwa. Mafunzo ya usimamizi wa ngombe na kilimo cha nyasi za kisasa zinazoimarisha afya ya mifugo vimewabadilishia maisha. Hayo yamefanikishwa na ufadhili na uelekezi wa shirika la maendeleo ya kilimo la Heifer International lililozindua mkakati mpya wa ujumuishi. Mpango huo unadhamiria kuimarisha miradi ya kilimo na mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.

Maziwa safi yanayopimwa kwa makini

Unapowasili kwenye kituo cha kupokea maziwa cha Lelchego,shughuli zimeshika kasi za kumimina na kupima maziwa kutoka kwa wakulima. Maziwa haya yanachukuliwa kutoka kwa wafugaji kila asubuhi kwa gharama ndogo ya usafirishaji. Jina la Lelchego ambalo ni la kikalenjin lina maana ya maziwa safi .

Salome Saina ni mfugaji na mwanachama wa chama cha Lelchego na anausifia mradi kwani, "Hii kampuni yetu nimefurahia sana. Wamenisaidia kabisa. Hata mzee huko nyumbani anafurahia.Tukilemewa kidogo anasema kimbia Lelchego uombe kakitu tuwakimbize hawa watoto waende shule.Lelchego walitupatia mbegu ya nyasi za super napier.Unachukua kidogo unapanda na kuongezea.Mimi sasa nimepanda kiasi ya eka moja ya nyasi hizo.

Wanawake wanavyojitoa kwenye uraibu wa dawa za kulevya

03:40

This browser does not support the video element.

"Tulipoanza wanawake walikuwa wachache sana"

Maziwa haya yanakaguliwa kwa makini kuhakikisha hakuna vijidudu vinavyomfikia mteja. Teknolojia ya kisasa inawawezesha kutimiza vigezo vya ubora wa maziwa vilivyowekwa.

Shirika la kuweka akiba na kukopesha la wafugaji wanaouza maziwa la Lelchego liliamua kuwashirikisha wanawake ambao kwa sasa wamefikia 800 kati ya wanachama wote alfu 2.

Wanawake wanachama hupata nafasi ya kunadi maziwa ya mchana ili kuliongeza pato lao. Idadi ya wanawake wanaouza maziwa kwa shirika hili imeongezeka na Heifer International imewashika mkono anaelezea Ruth Kosgei.

"Kuna wakati tulisaidiwa na Heifer International tukaweza kuwapa wanawake mafunzo na usimamizi bora wa ngombe wa maziwa. Kitamaduni,wanawake hujukumika nyumbani tu lakini umiliki wa ngombe ni wa mzee wa boma.Lakini kupitia mradi tumewashirikisha kina mama kwenye mambo ya biashara ya maziwa. Hiyo imesaidia kwani sasa wanataka kuhusika na biashara hii.Tulipoanza wanawake walikuwa wachache sana", alisema Kosgei. 

Mkakati wa kunyanyua wakulima wadogo na jamii

Mkulima wakiwasilisha maziwa kwenye kituo cha mapokezi cha chama cha Lelchego katika kaunti ya Uasin Gishu.Jina la Lelchego la jamii ya Kalenjin lina maana ya maziwa safiPicha: Thelma Mwadzaya/DW

Shirika la maendeleo ya kilimo la Heifer International limezindua mkakati mpya P4C wa kuimarisha miradi ya wakulima wasiopungua laki 6 wadogo kuoitia ufadhili na mafunzo kwenye vikundi .

Mkakati huo wa miaka 5 unapanua wigo na kujumuisha mafunzo ya kilimo na ufugaji hususan kwa wanawake na vijana. Agnes Kavatha ni meneja wa ubunifu na vijana na anakiri wanawake wemesogezwa karibu.

"Kupitia mafunzo yetu, tumeweza kuonyeshwa umuhimu wa kuhusisha kila mtu katika kilimo na miradi ili jamii yote au familia iweze kufaidika .Kwa mfano, tumeweza kuona kuwa mhusika mkuu,mzalishaji katika kila boma, yule anayelisha ngombe na kuzikama aghalabu ni mwanamke ila mmiliki wa mifugo ni mwanamume.Ili uweze kupata faida kwa wote, muhimu uwashirikishe wote ndio wapate motisha ya kufanya ile kazi,"

Nyasi za kisasa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Makopo matupu yaliyokuwa na maziwa yaliyowasilishwa kwenye kituo cha Lelchego cha kupokea maziwaPicha: Thelma Mwadzaya/DW

Ufugaji wa ngombe unaimarika pale nyasi za kisasa zilizo na virutubishi zinatumika.Wanawake wa Nandi wamepata nafasi kujifunza kuhusu kilimo cha nyasi za kisasa kuzitumia wakati wa kiangazi ili maziwa yasikosekane ambalo ni lengo kuu la Heifer International la maisha kuimarika kwa ujumla.

Clarice Bugo-Kionge ni mkurugenzi wa Heifer International nchini Kenya na anasisitiza kuwa mkakati mpya wa P4C unakuza ufanisi wa miradi ambayo imeleta tija kwa kujumuisha pia teknolojia na mbinu za kisasa za kuhimili mabadiliko ya tabia nchi ukizingatia kuwa,"Juhudi zetu zinajikita katika kuimarisha miradi ya kufuga ngombe wa maziwa,kuku, wa nyama na mboga na matunda ambavyo ni vipengee muhimu vya kutimiza moja kwa moja nadharia ya 2030 ya kuimarisha kilimo kuwa biashara ya kisasa ya kutegemewa.Mpango huo pia unapanua wigo kuzijumuisha jamii za wafugaji wa kuhamahama."

Mpango huo pia unadhamiria kuimarisha uwezo wa kifedha wa biashara za wakulima wasiopungua laki sita katika kaunti 26. Dhamira ya mkakati huo mpya utakaogharimu shilingi bilioni 12.4 ni kuimarisha kilimo kuwa biashara ya kisasa ya kutegemewa. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW