Biashara ya nje ya silaha za Ujerumani Magazetini
26 Oktoba 2016Tuanzie lakini na ripoti kuhusu biashara ya nje ya silaha za Ujerumani. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika: "Watu wengi wanaokufa vitani,hawafi kwasababu ya kupondwa na vifaru,kuripuliwa na maguruneti au mabomu yanayovurumishwa na ndege za kivita. Mauti yanasababishwa zaidi na bunduki za rashasha na silaha nyengine za aina hiyo. Ripoti kuhusu biashara ya silaha iliyochapishwa na serikali kuu ni kipimo timamu cha jinsi Ujerumani inavyoweza kufungua njia ya watu kuuwawa katika mizozo. Kwa namna hiyo mtu atafanya vizuri kuzimulika nchi kumi zinazopokea silaha zaidi kutoka Ujerumani. Nne kati ya hizo zinakutikana katika maeneo ya mizozo-Mashariki ya kati sawa na Afrika Kaskazini na baadhi ya nchi hizo zinakumbwa na mizozo ya kijeshi dhidi ya majirani zao.
Enzi za kutosafirisha silaha katika maeneo ya mizozo zimeshapita
Gazeti la "Der neue Tag" linasema zile enzi za Ujerumani kutotuma silaha katika nchi za mizozo zimeshapita. Gazeti linaendelea kuandika: "Kwa miaka kadhaa sasa kila ripoti kuhusu biashara ya silaha ya Ujerumani inakuwa inaonyesha nani ni nani katika zile nchi na hasa zile zinazokumbwa na mizozo ya umwagaji damu au zile zinazotajwa kuwa na tawala za kimabavu. Hata mnamo nusu ya mwanzo ya mwaka huu,silaha za Ujerumani na vifaa vyengine vya kijeshi havikupelekwa pekee katika nchi wanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO, bali pia nchini Algeria, Saud Arabia, nchi za falme za kiarabu au Iraq. Orodha ya nchi hizo inabainisha kwa mara nyengine tena kwamba kanuni za kale zinazokataza Ujerumani kutuma silaha katika maeneo ya mizozo, hazifai tena.
Baadhi ya wakimbizi waitumia vibaya imani ya wenyeji wao
Opereshini kubwa imefanywa na polisi jana katika miji ya majimbo matano ya shirikisho, dhidi ya vijana walioingia humu nchini na kuomba kinga ya ukimbizi. Wanatuhumiwa kugharimia ugaidi. Gazeti la mjini Cologne,"Kölner Stadt Anzeiger" linaandika: "Watuhumiwa wote 14,wake kwa waume,ambao kwa mujibu wa ripoti,wanatuhumiwa kugharimia opereshini za kigaidi,wanatokea Chechnya. Na wote ni wakimbizi.Yeyote yule mwenye imani na watu wanaokuja kuomba hifadhi nchini Ujerumani,hatoacha kuingiwa na hamu. Dhahir ni kwamba maafisa wa usalama hawakukosea licha ya kulaumiwa. Wimbi la wakimbizi linasababisha pia tatizo kwa usalama. Kwa wale wenye imani,wakarimu kuelekea wakimbizi,hizo si habari nzuri . Na habari hizo zitazidi kupalilia mtengano na watu kukata tamaa."
Wajerumani wanaridhika na hali yao ya maisha
Ripoti yetu ya mwisho inahusu ripoti inayochambua ubora wa hali ya maisha nchini Ujerumani. Ripoti hiyo imesema kwa jumla wajerumani wanaridhika na hali yao ya maisha. Lakini gazeti la "Trierischer Volksfreund" linaandika: "Kile ambacho wananchi wangependelea kukipata pindi wangeulizwa waseme wanachokitaka, kingeweza kujulikana hata bila ya gharama kubwa kubwa. Seuze tena wataalam tangu zamani wamekuwa wakijishughulisha na mada hiyo na hata bunge la shirikisho Bundestag limeshawahi kujadili ripoti ya tume maalum, iliyochapishwa miaka minne iliyopita; ilikuwa na kurasa 844. Hii leo inakuja ya kurasa 240 kutoka ofisi ya kansela na ambayo haina lolote jipya.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga