1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bibi Angela Merkel aongoza chupu-chupu tu

22 Septemba 2009

Uchaguzi wa Ujerumani jumapili hii:

Angela Merkel Ankunft Gipfel in Brüssel
Kanzela Merkel.Picha: AP

Uchaguzi wa Ujerumani ukinyemelea Jumapili hii,Septemba 27, kule kuongoza usoni kwa Kanzela Angela Merkel, kunazidi kupungua huku ishara zikionesha kwamba, huenda akalazimika kuingia tena katika serikali nyengine ya muungano wa vyama vikuu (Grand-coalition)-serikali ambayo huenda ikapepesuka katika kuikwamua Ujerumani kutoka msukosuko wa sasa wa kiuchumi.

Kanzela Merkel alitumai mara hii kuweza kuepuka kuunda tena serikali ya muungano kati ya chama chake cha kihafidhina cha mrengo wa kulia CDU/CSU na kile cha kijamaa cha SPD cha mrengo wa shoto.Bibi Merkel anasema kwamba, angependa kuepusha serikali ya aina hiyo kwavile, isingekuwa imara na ingekumbwa na matatizo ya kupitisha sera zinazohitajika kuukwamua uchumi ulio mkubwa kabisa barani ulaya.Bibi Merkel angehiyari kushirikiana na chama cha kiliberali cha Free Democratic party (FDP) badala ya SPD; na kuunda serikali ya mrengo wa kati na kulia ambayo ingepunguza malipo ya kodi za mapato na kutawala bila ya shida.Uchunguzi wa maoni wa kituo cha FORSA kwa niaba ya kituo cha TV cha RTL , umeonesha chama chake cha kihafidhina kina wingi ingawa sio wa kutosha sana kuifikia shabaha hii.

"Hakuna uhakika kabisa"-alisema mkurugenzi wa kituo cha taftishi za maoni cha FORSA Bw.Manfred Guellner.Akaongeza, "Wahafidhina wanazidi kudhofika na wajamaa wa SPD wanawachukulia wapigakura wao na wana waandaa wapigakura wao kwenda kupiga kura."

Uchunguzi wa hivi punde wa maoni, umeupa muungano wa wahafidhina unaoongozwa na Bibi Merkel pointi 10 usoni kuliko wapinzani wake wakubwa na washirika wa hivi sasa serikalinii-Social Democratic Party (SPD).Hii ina maana kwamba, Bibi Merkel hana wasi wasi wa ushindi kwa awamu yake ya pili ya utawala.

Lakini kambi yake ya mrengo wa kati na kulia, iko pointi 1 mbele kuliko vyama vitatu vyengine kwa pamoja na hii inazusha kitisho cha kubidi kuunda tena serikali ya muungano wa vyama vikuu kama ya sasa.

Hiyo ni serikali ambayo wachambuzi wanadai haitafanya kazi kwa maskizano makubwa kuliko hii iliotangulia inayotawala Ujerumani tangu 2005.Inabashiriwa pia kuwa huenda pia isidumu kipindi kizima cha utawala.

Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, chama cha kijamaa cha SPD kina pointi 26% na hicho ni kima cha juu kufikia tangu kupita miezi kadhaa.

Mpinzani mkuu wa Kanzela Merkel, mtetezi wa wadhifa wa ukanzela, waziri wa nje Frank-Walter Steinmeier ametiwa moyo na mafanikio ya karibuni ya chama chake na anatumai chama chake chaweza kurudi tena kutia fora dakika za mwisho kama kilivyofanya wakati wa uchaguzi wa 2002 na tena 2005.

Hatahivyo, washirika wa Bw.Steinmeier wa kuunda serikali ya muungano si wengi.Matumaini bora kabisa anayoweza kuweka, ni kuendelea waziri wa nje chini ya Bibi Merkel huku chama chake cha SPD kikiwa mshirika mdogo.Kwani, Bw.Steinmeier ameondoa uwezekano wa kushirikiana na chama cha mrengo wa shoto zaidi cha Linke kutokana na tofauti kubwa za sera kati yao.Chama cha shoto (Linke) kinawajumuisha wakoministi wa zamani na kinataka kurejesha askari wa Ujerumani nyumbani kutoka Afghanistan.

Muandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW