Bibi Obama ampigia debe Rais Obama
5 Septemba 2012Bibi Obama amekiri kuwa mabadiliko ambayo mumewe Barack Obama aliahidi wakati wa kampeini ya wadhifa wa urais miaka minne iliyopita hayajatimizwa kikamilifu lakini akawaomba wapiga kura kumpa miaka mingine minne ili kuuimarisha uchumi wa Marekani unaoyumbayumba.
Michelle Obama ndiye aliyekuwa wa kwanza kumtetea mumewe katika siku ya kwanza ya mkutano huo wa siku tatu ambao utakamilika kwa hotuba ya Obama kesho Alhamisi ili kukubali uteuzi wa chama cha Democratic wa kupambana na Mitt Romney katika uchaguzi wa uraisi tarehe sita Novemba.
Bibi Obama alisema "Kama rais, utapata ushauri wa kila aina kutoka kwa watu tofauti, lakini unapohitajika kufanya uamuzi wako kama rais, kinachokuongoza ni maadili na maono yako pamoja na uzoefu wa maisha, mambo yanayokufanya uwe jinsi ulivyo"
Katika kinyang'anyiro ambacho ni kikali kutabiri zikiwa zimebaki wiki tisa kabla ya Wamerakani kupiga kura, Obama anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa Republican Mitt Romney kwa sababu ya kudorora uchumi pamoja na asilimia 8.3 ya ukosefu wa ajira.
Rais huyo anajaribu kutumia mkutano huu mkuu kufufua tena msisimko uliombeba hadi katika ushindi wa mwaka wa 2008 lakini akakiri kwa mwaandishi wa habari mmoja wa televisheni ya Colorado kuwa hajatimiza alicholenga kufanya katika muhula wa kwanza.
Michelle Obama amesema na hapa namnukulu “kwa Barack, mafanikio siyo kiasi cha pesa ambacho unapata, ni kuhusu tofauti unayoweka katika maisha ya watu.” Wazungumzaji katika kongamano hilo walimshambulia Romney kuhusu rekodi yake ya kibiashara, kukataa kulipa kodi zaidi na kwa kuongoza vita vya Warepublican dhidi ya wanawake.
Wademocrat waliangazia mafanikio ya Obama wakati wa muhula wake wa kwanza, wakigusia masuala kama vile kuamuru operesheni iliyomuua kiongozi wa al Qaeda Osama bin Laden, kuiokoa sekta ya magari, huku wakiwakumbusha wapiga kura kuhusu matatizo ambayo Obama alikabiliwa nayo wakati alipoingia madarakani.
Warepublican wanalalamika kuwa Wademocrat wanajaribu kushughulikia tu masuala ya wanawake na mada nyengine ili kukwepa kuzungumzia uchumi wa nchi hiyo.
Obama anaingia katika mkutano huo mkuu akiwa na alama nyingi kutoka kwa wapiga kura kuhusu masuala ya kibinafsi lakini akikabiliwa na shaka kuhusu namna anavyoshughulikia uchumi wa Marekani. Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na shirika la habari la Reuters, kwa jumla Romney alimpiku Obama na asilimia 46 kwa asilimia 45 miongoni mwa wapiga kura.
Huku Wademocrat wakiwa na wasiwasi kuhusu kinyang'anyiro kikali, Bibi Obama aliwataka wanaharakati wa chama kumpigia debe rais. Obama atatoa hotuba yake katika uwanja wa kandanda utakaojaa watu 74,000 usiku wa kesho Alhamisi.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Josephat Charo