1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aahidi kuilinda Israel na vitisho vya Iran

2 Agosti 2024

Rais wa Marekani Joe Biden amefanya mazungumzo usiku wa Alhamisi na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kumhakikisha kuwa Marekani iko tayari kulinda usalama wa Israel dhidi ya vitisho vyote vya Iran.

Washington - Joe Biden akiwa na Benjamin Netanyahu
Rais wa Marekani Joe Biden (Kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Washington: 25.07.2024Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Biden amesema Marekani iko tayari kukabiliana na vitisho hasa kutoka makundi ya kigaidi ya Hamas, Hezbollah na Wahouthi ambayo yanafadhiliwa na Iran.

Hayo yameelezwa na Ikulu ya White House baada ya kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Hamas  Ismail Hanniyeh  mjini Tehran pamoja na kamanda wa kijeshi wa Hezbollah Fuad Shukr mjini Beirut.

Makamu wa rais na mgombea urais wa Marekani kupitia tiketi ya chama cha Democratic Kamala Harris, alijiunga pia na mazungumzo hayo na kwa pamoja wakasisitiza kuwa juhudi zinaendelea ili kupunguza hali ya mvutano mkubwa huko Mashariki ya Kati.

Javad Zarif ateuliwa kuwa Makamu wa rais wa Iran

Rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian (kulia) akiwa na Javad Zarif aliyemteua kuwa makamu wake wa rais. Picha: Rouzbeh Fouladi/ZUMAPRESS/picture alliance

Rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian amemteua Javad Zarif kuwa makamu wake wa rais. Mwanadiplomasia huyo mwenye msimamo wa wastani aliwahi pia kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kati ya mwaka 2013 na 2021.

Shirika la habari la ISNA limearifu kuwa Mohammad Javad Zarif ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa pia mshauri wa rais, atamsaidia Pezeshkian katika masuala muhimu ya kimkakati.

Soma pia: Blinken aitaka Mashariki ya Kati kujizuia kuongeza mzozo

Zarif alikuwa mpatanishi mkuu wa Tehran katika mkataba wa kihistoria wa kimataifa wa nyuklia na mamlaka za kimataifa mnamo mwaka 2015, na anafahamika kama mtetezi wa mahusiano bora na nchi za Magharibi na anayeunga mkono mazungumzo ya moja kwa moja na  Marekani.

Wachambuzi wanasema huenda Javad Zarif akasaidia kupunguza hali mvutano kati ya Iran na Israel baada ya mauaji ya Kiongozi wa Hamas na kamanda wa kijeshi wa kundi la Hezbollah la Lebanon.

Rais Pezeshkian alilaani mauji ya viongozi hao na akaapa kulipiza kisasi huku Javad akilaani pekee na kujizuia kutoa aina yoyote ya vitisho kwa Israel.

Vyanzo: (Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW