Biden aahidi ushirika thabiti na Afrika
15 Desemba 2022Rais Joe Biden amesema hayo kwenye mkutano wa kilele kati ya Marekani na Afrika jijini Washington, unaohudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa mataifa 49 ya Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo wa siku tatu na wa kwanza tangu rais Barack Obama alipowaalika viongozi wa Afrika mwaka 2014, Biden alijizuia kuitamka China, ingawa aliweka wazi kwamba Marekani itachukua mkondo tofauti. Akasema, Marekani inataka ushirika utakaochochea mafanikio na fursa za pamoja na si wa kuchochea utegemezi.
Marekani imekuwa nyuma ya China katika suala la uwekezaji Barani Afrika kunakogombaniwa na mataifa yenye nguvu duniani.
"Kama viongozi, watu wetu wanatutia moyo. Wanatukumbusha kuhusu fursa zilizopo ndani ya uwezo wetu. Kuna fursa nyingi tukishirikiana. Wanatuambia ukweli mgumu ambao tunalazimika kuusikiliza. Na wakati mwingine tunapata shida kuwasikiliza. Wanatupa changamoto ya kuishi kulingana na maadili yaliyoko. Katika miaka yangu ya kujihusisha na siasa na uhusiano wa kimataifa, sijawahi kuwa na matumaini kama sasa, na ninamaanisha hili kwa dhati," Alisema.
Akasisitiza, Marekani ikifanikiwa na Afrika inafanikiwa, na ulimwengu kwa ujumla wake na kuwaambia viongozi hao kwamba mabadiliko ya kiuchumi ya Afrika yanategemea utawala bora, watu wenye afya na nishati ya uhakika na nafuu.
Serikali ya Biden imetangaza msaada wa zaidi ya dola bilioni 55 na jana Jumatano iliwaalika wafanyabiashara wa Marekani na Afrika ambo pia waliahidi zaidi ya dola bilioni 15 kupitia makubaliano ya kibiashara.
Biden baadae aliwaalika viongozi hao kwenye hafla ya chakula cha jioni katika ikulu ya White House ambako alizungumzia ukatili wa kiwango cha juu aliouita "dhambi ya asili" uliofanywa na taifa hilo enzi ya utumwa, huku kwa upande mwingine akisifu mchango wa waAfrika wanaoishi nchini humo.
Biden aidha alitangaza msaada wa dola milioni 100 utakaotumika kwenye eneo la nishati safi, na msaada mwingine uliotangazwa na Ikulu ya White House wa dola milioni 800 utakaofadhili maendeleo ya kidijitali barani humo na kusema taifa hilo limejizatiti katika kusaidia ukuaji wa kila sekta barani Afrika.
Sikiliza Zaidi:
Katika hatua nyingine, rais wa Rwanda Paul Kagame alijitenga na mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akisema, hayajasababishwa na Rwanda na kwa hivyo sio tatizo la Rwanda, ni tatizo la Kongo. Alisema hayo nje ya mkutano huo wa kilele wa viongozi wa Afrika, huko Washington.
Uasi wa wanamgambo wa M23 kwenye eneo hilo umesababisha vifo vya mamia ya watu na unaaminika kufadhiliwa na Rwanda, ingawa Kagame anakana kuhusika, akisema hawezi kubebeshwa lawama za Wakongo wenye asili ya Rwanda walioko Kongo ambao wananyimwa haki zao kama raia.