Biden aanza ziara yake ya kwanza ya kigeni
10 Juni 2021Akiwahutubia karibu wanajeshi 1,000 na familia zao katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Uingereza, Biden amesema atawasilisha ujumbe wa wazi kwa Rais wa Urusi Vladmir Putin watapokutana wiki ijayo baada ya kuhudhuria mikutano tofauti ya kilele na NATO na G7 na viongozi wa UIaya.
Biden amesema amedhamiria kuyajenga upya mahusiano ya Marekani na Ulaya na kurekebisha mahusiano na Urusi baada ya miaka minne migumu chini ya Rais Mrepublican Donald Trump, ambaye maamuzi yake ya kuongeza ushuru kwa bidhaa na kujiondoa kwenye mikataba yaliharibu mahusiano na washirika wakuu. Biden atakuwa Uingereza hadi Jumapili
Kwa washirika wengi wa Marekani, Biden ni kiongozi wanayemtazama kwa jicho la faraja. Na sababu kubwa ni kwamba mtangulizi wake alisababisha mvurugano mkubwa mara kwa mara,akiushutumu muungano wa kijeshi wa NATO kwamba umekuwa ukiitumia vibaya Marekani, na kuitukana Umoja wa Ulaya, na wakati mmoja kufikia hatua mpaka ya kuondoka kwenye mkutano wa kilele wa G7 uliofanyika Canada mwaka 2018.