1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Biden aapa kuilinda Taiwan endapo China itaivamia

22 Oktoba 2021

Rais Joe Biden wa Marekani amesema nchi yake itakilinda kisiwa cha Taiwan, endapo China itakivamia, kauli ambayo ni kinyume na sera rasmi ya Marekani na inayoogeza mtafaruku wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.

USA Präsident Joe Biden
Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Akijibu swali la kituo cha CNN mjini Baltimore siku ya Alhamis (Oktoba 21) endapo Marekani itasimama upande wa Taiwan, Biden alisema watafanya hivyo kwa kuwa ndiyo ahadi waliyoweka. 

Rais huyo wa Marekani alisema hakuna sababu ya watu kuhofia uwezo wa kijeshi wa taifa lake, "kwani mataifa makubwa kama vile China na Urusi yanajuwa kuwa Marekani ndilo taifa lenye nguvu kubwa kabisa za kijeshi kwenye historia ya ulimwengu."

Kauli hiyo ya Biden inakuja ikiwa ni siku mbili tu tangu mteule wake wa nafasi ya Balozi wa Marekani nchini China, Nicholas Burns, kuonesha msimamo mkali dhidi ya China wakati wa kikao cha Baraza la Seneti cha kuidhinisha uteuzi wake, akisema kuwa "mauaji ya maangamizi katika mkoa wa Xinjiang", ukandamizaji jimboni Tibet na uchokozi dhidi ya Taiwan lazima vikome. 

Makhsusi kabisa kuhusu Taiwan, ambayo China inaichukulia kuwa ni eneo lake lililoasi, Burns alisema bunge la Marekani lina wajibu wa kukilinda kisiwa hicho kwa gharama yoyote.

"Kwa kuzingatia kile ambacho China imeshakifanya na kauli zake tata kuelekea Taiwan, nadhani baraza la Congress na serikali wana kila haki ya kuuendeleza zaidi ushirikiano wa kiusalama na kuongeza idadi ya silaha kwa Taiwan. Hicho ndicho kitu muhimu kabisa tunachoweza kufanya." Alisema Burns akiwa mbele ya kamati ya Seneti.

China yaja juu

Rais Xi Jinping wa China.Picha: Li Xueren/Xinhua/picture alliance

Kauli hiyo ya Burns iliikasirisha sana China, ambayo jana kupitia msemaji wake wa mambo ya kigeni, Wang Wenbin, ilimtaka mteule huyo wa nafasi ya balozi wa Marekani, kuchunga ulimi wake panapohusika mambo ya ndani ya China.

"Mambo ya Taiwan, Xinjian na Hong Kong ni mambo ya ndani ya China na hakuna mgeni yoyote anayepaswa kuyaingllia. Sera ya China moja ni msingi wa kisiasa wa mahusiano ya China na Marekani, na Taiwan ni sehemu isiyotenganishika ya mamlaka ya China. Marekani imeweka ahadi ya wazi kwa China kwenye andiko lake la tarehe 18 Agosti kuhusiana na kuacha kuizuia Taiwan silaha, na lazima iheshimu maneno yake." Alisema Wang mbele ya waandishi wa habari mjini Beijing.

Taiwan ina wasiwasi wa kuvamiwa

Rais Tsai Ing-wen wa Taiwan.Picha: Daniel Ceng Shou-Yi/picture alliance

Waziri wa Ulinzi wa Taiwan, Chiu Kuo-cheng, alisema mwezi huu kwamba, hali ya wasiwasi imezidi kutanda nchini mwake, akiongeza kwamba China itakuwa na uwezo wa kuivamia rasmi kufikia mwaka 2025.

China inashikilia kuwa Taiwan ni eneo lake ambalo litachukuliwa hata kwa nguvu itakapobidi, huku Taiwan ikisema ni taifa huru ambalo liko tayari kutetea mipaka na demokrasia yake.

Kisheria, serikali ya Marekani inatakiwa kuipa Taiwan njia za kujilinda yenyewe, lakini kwa muda mrefu imekuwa ikifuata sera ya "utata wa kimkakati" juu ya iwapo itaingilia kijeshi kuilinda Taiwan kama itavamiwa na China.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW