Biden aendelea na mipango ya kuunda serikali
11 Novemba 2020Joe Biden anapanga kukutana leo Jumatano na kikundi cha washauri wake, ambao wanamsaidia kuweka msingi wa utawala mpya, na kumuandaa kula kiapo cha kuchukua madaraka aifikapo Januari 20 mwakani.
Miongoni mwa washauri hao ni wataalamu wa masuala ya kibenki na kifedha, wanaotoka chama chake cha Democratic pamoja na wale wenye mrengo usio wa kihafidhina, akinuia kuakisi mjadala unaoendelea ndani ya chama hicho juu ya namna ya kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.
Rais huyo mteule anawatumia watu waliopangilia sheria kali za kimazingira wakati wa utawala wa Rais Barack Obama.
Licha ya Rais Trump na maafisa wengi wa chama cha Republican kuendelea kukaidi kuyakubali matokeo ya uchaguzi wa Novemba 3, uchunguzi wa maoni ya raia uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa ushirikiano na shirika la utafiti la Ipsos, na ambao ripoti yake ilichapishwa jana Jumanne, umeonyesha kuwa asilimia 80 ya Wamarekani, wakiwemo nusu ya Warepublican, wanamkubali Biden kama mshindi halali. Soma zaidi Biden azidi kupongezwa
Kuendelea kupinga matokeo ni sumu kwa Demokrasia
Mmoja wa Warepublican hao ni seneta Mitt Romney, ambaye amesema kuendelea kupinga matokeo ni doa kwenye sura ya Marekani.
''Sielewi ninapowasikia watu wanaosema uchaguzi ulikuwa na mizengwe na wizi. Kwa maoni yangu, hilo sio sahihi, na pili, ni hatari katika mchakato wa uhuru, kwa sababu macho yote ya dunia yanaitazama Marekani, kuangalia jinsi tunavyoushughulikia uchaguzi huu.'' amesema Seneta Mitt Romney.
Kwa upande mwingine, Rais Donald Trump anaendeleza mchakato wake wa kimahakama, akishikilia madai yake ya udanganyifu katika uchaguzi alioupoteza, bila hata hivyo kuambatanisha malalamiko yake na ushahidi ulio bayana.
Tayari majaji wamekwiyatupilia mbali malalamiko ya Trump katika majimbo ya Michigan na Georgia, na wataalamu wa sheria wanasema mashitaka yake yana nafasi finyu ya kuweza kubadilsha matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi Biden.
Licha ya hali hiyo lakini, sehemu kubwa ya maafisa wa chama cha Republican wameendeleza mshikamano na Rais wa Trump, wakisema anayo kila haki ya kulalamika pale anapoamini kuwa hakutendewa haki.
Huku hayo yakijiri, shughuli za kuhesabu kura bado hazijakamilika katika majimbo kadhaa yaliyokuwa na uishindani mkali. Rais Trump anaongoza katika jimbo la North Carolina, huku Biden akiwa mbele katika majimbo ya Georgia na Arizona, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la uchunguzi la Edison Research.
/rtre, ape