1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aiahidi Urusi majibu makali ikiivamia Ukraine

13 Februari 2022

Rais wa Urusi Vladmir Putin amezungumza kwa simu na rais wa Marekani Joe Biden, katika juhudi za karibuni kutuliza mzozo. Mazungumzo hayo ya simu yamefanyika wakati serikali zaidi zikiwaambia raia wake kuondoka Ukraine.

Ukraine Russland Konflikte | US-Präsident Joe Biden
Picha: The White House via AP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden na rais wa Urusi Vladmir Putin walizungumza Jumamosi, wakati mzozo juu ya Ukraine ukifikia hatua ya kutisha, kufuatia matamshi ya Washington kwamba Urusi ilikuwa inakaribia kuivamia Ukraine.

Biden alizungumza na Putin kutokea Camp David, ambalo ni eneo la mapumziko la rais wa Marekani jimboni Maryland. Mazungumzo hayo ya simu yalidumu kwa zaidi ya saa moja.

Soma pia:Marais wa Marekani na Urusi kuzungumza kwa simu juu ya mgogoro wa Ukraine

Biden alionya kwamba Marekani na washirika wake watajibu kwa ukali na kuchukua hatua za haraka na za gharama kubwa iwapo Urusi itafanya uvamizi, kwa mujibu wa ikulu ya White House. Alimuambia Putin kwamba kuivamia Ukraine kutasababisha "mateso makubwa ya kibinadamu."

Rais Joe Biden (kushoto) amemuonya Putin (kulia) juu ya hatua kali na za haraka endapo nchi yake itaivamia Ukraine.Picha: Jim Watson/Grigory Dukor/AFP

Marekani ipo tayari kushiriki katika diplomasia na Urusi kuhusu hali nchini Ukraine, lakini vivyo hivyo "iko tayari kwa uwezekano mwingine," Biden alimuambia Putin.

Afisa wa serikali ya Marekani, akizungumza kwa sharti la kutotajw ajina, aliwamabia maripota kwamba mazungumzo yalikuwa ya "kiueledi na yakinifu," lakini hakukuwa na mabadiliko makubwa katika mambo yanayojitokeza kwa wiki kadhaa sasa."

Hii ilikuwa ndiyo mara ya kwanza tangu mwezi Desemba, kwa viongozi hao kuzungumza.

Soma pia:Marekani yasema Urusi inaweza kuivamia Ukraine muda wowote

Kuafuatia simu hiyo, ikulu ya Kremlin ililaani kile ilichokiita "kilele cha kiwewe" cha Marekani kuhusu mgogoro wa Ukraine, lakini ilisema Putin na Biden walikubaliana kuendeleza majadiliano.

Mshauri wa juu wa masuala ya kigeni wa Kremlin, Yury Ushakov, alisema Putin alilalamika kwamba mataifa ya magharibi yamekuwa yakiipa silaha Ukraine na kwamba mamlaka za Kyiv zimekuwa "zikihujumu" makubaliano ya amani yalioratibiwa na mataifa hayo ya magharibi kukomesha mzozo wa miaka kadhaa mashariki mwa Ukraine.

Macron, Scholz, Zelenskyy pia washirikishwa

Simu ya viongozi hao ilikuja wakati ambapo mataifa kadhaa ya Ulaya yamewahimiza raia wao kuondoka Ukraine haraka iwezekanavyo. Siku ya Jumamosi, Marekani iliwaruhusu wafanyakazi wasio wa dharura kwenye ubalozi wake mjini Kyiv kuondoka na kubakisha timu ndogo tu kwenye mji wa magharibi wa Lviv.

Wa Ukraine waliandamana mjini Kyiv dhidi ya kuongezeka kwa mzozo wa miaka 8 sasa na Urusi.Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova pia alisema wafanyakazi wa kidiplomasia wa Urusi wataondoka kutoka ubalozi wa nchi hiyo mjini Kyiv, na kuacha tu wafanyakazi wachache katika mji mkuu wa Ukraine.

Kabla ya simu ya Jumamosi na Biden, Putin pia akizungumza kwa njia ya simu na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Wawili hao walikuwa wamekutana mjini Moscow mapema katika wiki kujaribu kutatua kile kinachoonekana kama mzozo mkubwa zaidi wa kiusalama kati ya urusi na mataifa ya magharibi tangu Vita Baridi.

Lakini mukhtasari wa simu hiyo uliowasilishwa na Kremlin uligusia kwamba hakukupigwa hatua kuelekea kutuliza hali. Ofisi ya Macron, wakati huo huo, ilisema "wawili hao walielezea shauku ya kuendelea kujadiliana."

Putin alijibu madai ya uvamizi unaokaribia wa Moscow dhidi ya Ukrane, akiyataja kuwa "uchokozi."

Ni upi uwezekano wa mzozo wa kivita?

Makabiliano kati ya mashariki na magharibi yanakuja wakati ambapo Urusi imelundika zaidi ya wanajeshi 100,000 kwenye mipaka ya Ukraine. Kwa sasa, Urusi inafanya luteka za kijeshi katika Bahari Nyeusi pamoja na mazoezi ya kijeshi nchini Belarusi, karibu na mpaka wa kaskazini wa Ukraine. Kremlina imesema haina nia ya kuivamia Ukraine.

Urusi yafanya luteka kubwa za kijeshi Belarus huku mzozo wa Ukraine ukizidi kushika kasi

01:49

This browser does not support the video element.

Kilichoongezea mazingira ya taharuki Jumamosi ni madai ya Urusi kwamba ilifukuza nyambizi ya Marekani iliyovuka na kuingia eneo lake la maji kaskazini mwa bahari ya pasisiki. Marekani ilikanusha madai ya Urusi, ikisema "hakuna ukweli" juu ya tuhuma hizo.

Mzozo unaoongozeka juu ya Ukraine na uwezekano wa kuzuka vita barani Ulaya vinaonekana kama mtihani mkubwa zaidi kwa siasa za kieneo kwa jumuiya ya kujihami NATO na Ulaya tangu Vita Baridi.

Zelensky aonya kuwa taharuki inawasaidia madui

Licha ya ishara zinazoongezeka kwamba hali huenda inaelekea kwenye kuzidi kwa uhasama, rais wa Ukraine aliwaambia waandishi habari siku ya Jumamosi kuwa ameshangazwa na duru ya karibuni zaidi ya maonyo na uondokaji kutoka serikali za magharibi.

Soma pia: NATO yasema Urusi lazima ifanye chaguo la suluhu katika mzozo na Ukraine

Zelensky alisema yeyote mwenye taarifa kuhusu uvamizi anapaswa kuifahamisha serikali ya Ukraine. Alisema taharusiki hivi sasa itawasaidia tu madui wa Ukraine. "Tunafahamu juu y ahatari zote," alisema. "Tunafahamu kwamba hatari zipo."

Rais wa Ujeruani Frank-Walter Steinmeier amemhimiza Putin kulegeza msimamo kuhusu suala la Ukraine.Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Steinmeier atoa wito kwa Urusi

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameonya juu ya uwezekano wa kutoka vita endapo Urusi itaivamia Ukraine.

"Tuko katikati mwa hatari ya mzozo wa kijeshi, vita mashariki mwa Ulaya," Steinmeier aliuambia mkutano maalumu uliomchagua kwa muhula wa pili, na kuongeza kuwa "Urusi inabeba dhamana ya hili."

"Namtolea wito rais (wa Urusi) Puti: Legeza msimamo kuhusu Ukraine na utafute nasi njia y akulinda amani barani Ulaya," alisema.

Chanzo: DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW