Mweleko wa siasa nchini Israel na Palestina
10 Machi 2010Makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden akiwa na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas, amelaani mipango ya Israel ya kutaka kujenga makaazi elfu moja mia sita katika kipande cha ardhi ilichokinyakua kutoka kwa Waarabu wa mashariki mwa mji wa Jerusalem.
Biden aliyezungumza akiwa katika eneo la Ramallah, Ukingo wa magharibi, alisema pande zote mbili zinafaa kuboresha mazingira ya mazungumzo wala sio kuyasambaratisha.
Aliongeza kusema kwamba uamuzi wa Israel kujenga makaazi mapya mashariki mwa Jerusalem unadumaza matumaini ya kupatikana amani na kuvuruga imani inayohitajika zaidi wakati huu ili kuwe na mazungumzo ya manufaa.
Kiongozi wa Wapalestina, Mahmoud Abbas pia amelaani hatua hiyo ya Israel na jitihada zake za kujenga makaazi 112 kwa walowezi wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi. Abbas alisema uamuzi huo wa Israel wa siku mbili zilizopita unahatarisha juhudi za amani za miezi iliyopita za kuanzisha tena mazungumzo ya upatanishi.
Wapalestina wananuia kuifanya mashariki mwa Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa waliloahidiwa.
Biden amesema anatarajia mikutano mjini Jerusalem na Ramallah itatoa fursa ambayo Israel na Palestina zimekubali kuendeleza mazungumzo ya upatanishi kwa muda wa miezi kumi na minne ijayo. Biden amesema pia kwamba hatimaye suluhisho la amani litakuwa uundwaji wa taifa huru la Palestina.
Biden akizungumza na waandishi wa habari amesema lengo la amani sio tu kwa manufaa ya Palestina na Israel bali pia kwa Marekani.
Uamuzi wa Israel wa kupanua makaazi kwa manufaa ya walowezi wa kiyahudi mashariki mwa Jerusalem ulilaaniwa pia na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon, Jumuiya ya Ulaya, jumuiya ya nchi za kiarabu na pia waziri wa ulinzi wa Israel.
Ban Ki Moon amesema uamuzi huo unakiuka sheria za kimataifa ilhali mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu, Amr Mussa akasema ukiukaji huo umefika kiwango ambacho hakiwezi kukubalika na Muarabu yeyote na kwamba Israel haijali mtu yeyote akiwemo mpatanishi na Wapalestina.
Taarifa kutoka kwa afisi ya waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak imeelezea kukasirishwa kwake na tangazo la upanuzi wa makaazi linasambaratisha mazungumzo ya amani na Wapalestina.
Ufaransa pia imeelezea msimamo wake kuhusu mustakabali wa Israel na wizara ya mambo ya nje imesema mipango ya ujenzi wa makaazi mapya ni haramu .
Mwandishi: Peter Moss/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo