1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden amkosoa Putin, aunga mkono mageuzi Umoja wa Mataifa

Josephat Charo
22 Septemba 2022

Rais wa Mareani Joe Biden ameituhumu Urusi kwa kuziendea kinyume sheria za kimatiaa kwa kuivamia Ukraine. Ameunga mkono kulifanyia mageuzi baraza la usalama kuongeza viti vya kudumu kwa bara la Afrika na Amerika Kusini.

US-Präsident Joe Biden spricht vor der UN
Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani ameituhumu Urusi kwa kuvunja sheria ya kimataifa bila aibu kwa kuivamia Ukraine, wakati alipoahidi mabilioni ya dola kwa ajili ya msaada wa chakula. Biden alitaka kutafuta kuungwa mkono na ulimwengu katika Umoja wa Mataifa saa chache baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kuamuru wanajeshi wa akiba kwenda vitani nchini Ukraine, hatua ambayo dola za Magharibi zimeieleza kuwa ya kukata tamaa.

"Tuzungumze ukweli. Mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa amemshambulia jirani yake na amejaribu kuifuta dola huru kutoka kwa ramani ya dunia. Urusi bila haya imevunja sheria muhimu za msingi za Umoja wa Mataifa. Sasa Urusi inawaita wanajeshi wa akiba wajiunge na vita Ukraine na Kremlin unaandaa kura za maoni kujaribu kuyatwaa maeneo ya Ukraine, hatua inayokiuka katiba ya Umoja wa Mataifa. Putin anadai alilazimika kuchukua hatua kwa sababu alitishwa, lakini hakuna aliyeitish Urusi. Na hakuna aliyetaka vita mbali na Urusi."

Biden ametangaza msaada wa dola bilioni 2.9 zinazonuiwa kushughulikia usalama wa upatikanaji wa chakula, ambao umekuwa mbaya tangu uvamizi wa Ukraine, msafirishaji mkubwa wa nafaka. Rais Biden pia ameunga mkono mageuzi ya kulitanau baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuongeza viti vya kudumu kwa nchi zinazoendelea. Amesema Marekani itaunga mkono wazo la kuongeza viti vya kudumu kwa bara la Afrika na Amerika Kusini, mbali na ahadi yake ya awali ya kuijumuisha Japan na India. Pia ameahidi kuwa Marekani itajizuia kutumia kura ya turufu, isipokuwa katika mazingira muhimu na ya lazima, kuhakikisha baraza la usalama la linabaki kuwa la kuaminika na lenye ufanisi.

Zelensky ataka Urusi iadhibiwe

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewahimiza viongozi wa dunia kuivua Urusi kura yake ya veto katika taasisi za kimataifa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, akisema wachokozi wanahitaji kuadhibiwa na kutengwa.

"Uhalifu umefanywa dhidi ya Ukraine na tunataka adhabu ya haki. Uhalfi ulifanywa dhidi ya mipaka ya dola letu, uhalifu ulifanywa dhidi ya maisha ya watu wetu, uhalifu ulifanywa dhidi ya heshima ya wanawake na wanaume wetu. Uhalifu ulifanywa dhidi a maadili yanayotufanya sote kuwa jamii ya Umoja wa Mataifa, na Ukraine inataka adhabu kwa kujaribu kuiba himaya yetu."

Rais Volodymyr Zelensky wa UkrainePicha: Igor Golovniov/SOPA/ZUMA/picture alliance

Zelensky alianza hotuba yake iliyosubiriwa kwa hamu kubwa kwa njia ya video katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa saa chache baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kutangaza amri ya kuwatumia wanajeshi wa akiba kuendeleza vita vyake dhidi ya Ukraine. Amri hiyo haikuwa na maelezo ya kina lakini maafisa wamesema wanajeshi hadi 300,000 wa akiba huenda wakatumiwa.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema anaitisha kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa umoja huo kuanza kupendekeza vikwazo vipya kushughulikia kitisho cha Urusi kutumia silaha za nyuklia nchini Ukraine na kura za maoni zinazoandaliwa katika maeneo manne ya Ukraine kuamua kujiunga na Urusi.

Ruto azungumzia ukame Kenya

Rais wa Kenya William Ruto ameipongeza hotuba ya Biden kuhusu mageuzi kama hatua muhimu katika muelekeo sahihi. Ruto pia amesema sehemu za Kenya zinakabiliwa na ukame mbaya katika kipindi cha miaka 40 na kuwaacha watu zaidi ya milioni 3 kukabiliwa na uhaba wa chakula. Katika hotuba yake ya kwanza katika hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa Ruto amesema maeneo yaliyoathiriwa yamepata mvua chache katika misimu mitatu mfululizo na usumbufu na changamoto katika minyonyoro ya ugavi wa chakula zimeifanya hali kuwa mbaya.

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ametahadharisha kwamba hata miezi michache ya vita inaweza kufuta miongo ya mafanikio katika mapambano ya kutokomeza umasikini. Hichilema amesema vita katika sehemu yoyote ya dunia ina athari hasi kwa shughuli za kiuchumi, hali ambayo inavuruga na kutatiza juhudi za pamoja za mapambano dhidi ya umasikini na njaa. Kiongozi huyo pia amezungumzia mfano wa athari za mabadiliko ya tabia nchi katika nchi yake, huku nusu ya Zambia ikikabiliwa na ukosefu wa mavuno na mimea ikifa kutokana na ukame mbaya, huku nusu nyingine ya nchi ikikabiliwa na mafuriko.

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema madai yaliyotolewa na rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tchisekedi katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa ni mchezo wa kulaumiana ambao hautatui matatizo ya ukanda wa maziwa makuu. Kagame amesema mashariki mwa Congo changamoto za hivi karibuni zimedhihirisha kwamba hali ya usalama haijabadilika ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka 20 iliyopita wakati ujumbe mkubwa kabisa na wa gharama kubwa wa Umoja wa Mataifa ulipotumwa kwa mara ya kwanza nchini humo.

(afp, ap)

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi