1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Biden amrai Netanyahu dhamira ya kulipa kisasi dhidi ya Iran

15 Aprili 2024

Rais wa Marekani Joe Biden amemtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufikiria kwa makini shambulizi lolote la Israel la kulipiza kisasi dhidi ya Iran pamoja na matokeo yake.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Biden pamoja na viongozi wenzake wa nchi saba tajiri duniani G7, waliujadili mzozo huo na kulaani shambulio la Iran. John Kirby msemaji kuhusu  usalama wa taifa katika ikulu ya White House amesema hawataki kuuona mzozo ukitanuka na wala hawataki kutafuta vita kamili na Iran huku akisema Marekani itaendelea kuisadia Israel kujilinda.

Uingereza nayo kupitia Waziri wake wa mambo ya kigeni David Cameron imetoa wito sawa na huo wa kuitaka Israel kutojibu mashambulizi ya Iran, baada ya nchi hiyo kuishambulia Israel kwa droni na makombora yaliyofanikiwa kudunguliwa kwa asilimia 99. 

Jana pia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wa dharura kufuatia shambulio hilo la Iran dhidi ya Israel na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akatahadharisha kwamba kanda hiyo iko ukingoni kutumbukia vitani.

Iran ilirusha makombora na droni zaidi ya 300 yalliyodunguliwa kupitia mfumo wa kujilinda na makombora wa Israel na pia usaidizi kutoka Marekani, Ufaransa na Jordan. Jamhuri hiyo ya kiislamu ilikuwa inajibu shambulizi linalodhaniwa kufanywa na Israel katika ubalozi wa Iran nchini Syria mnamo Aprili mosi.