1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden amtuhumu Putin kwa mauaji ya halaiki nchini Ukraine

Sylvia Mwehozi
13 Aprili 2022

Rais wa Marekani Joe Biden amevitaja vita vya Urusi nchini Ukraine kuwa mauaji ya halaiki, yanayolenga kuiangamiza Ukraine, kauli iliyopongezwa na rais Volodymyr Zelensky.

Ukraine | Krieg | Massengrab in Buzova
Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Akizungumza katika hafla moja huko Iowa, alipokuwa akielezea kupanda kwa gharama ya nishati kutokana na mzozo huo, Biden alidokeza kwamba Putin anatekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Ukraine. Kauli ya Biden imepongezwa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, ambaye amekuwa akiwahimiza viongozi wa magharibi kutumia neno hilo kuelezea uvamizi wa Urusi katika nchi yake. Ukraine imekuwa ikiishutumu Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita, hata kabla ya kugunduliwa kwa miili ya watu wanaodaiwa kuuawa mjini Bucha. Chini ya sheria za kimataifa, mauaji ya halaiki huchukuliwa kama dhamira ya kuharibu kwa ujumla au sehemu ya taifa, kabila, rangi au kikundi cha kidini.

Mshirika wa karibu wa Putin akamatwa

Shirika la ujasusi la Ukraine SBU limedai kumshikilia mwanasiasa wa upinzani nchini humo Viktor Medvedchuk, ambaye anaunga mkono Urusi na mshirika wa karibu wa rais Vladimir Putin. SBU imechapisha picha za mwanasiasa huyo akiwa katika hali ya uchovu na kufungwa mikono akiwa amevalia sare za Ukraine. Kigogo huyo mwenye umri wa miaka 67 anachukuliwa kuwa mtu muhimu katika mzozo kati ya Moscow na Kyiv kwa miaka mingi. Uhusiano wake na Putin wakati mwingine ulimfanya kuwa kama mpatanishi. Mnamo Mei mwaka jana Medvedchuk aliwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa mashtaka ya uhaini, lakini alitoroka kabla ya Urusi kuishambulia Ukraine.

Viktor Medvedchuk manasiasa wa upinzani wa UkrainePicha: Stringer/Sputnik/dpa/picture alliance

Rais Vladimir Putin aliapa kwamba Urusi itaendeleza mashambulizi yake hadi pale malengo yake yatakapotimiana kusisitiza kuwa kampeni inaendelea vyema, licha ya kupata upinzani mkali kutoka Kyiv. Vikosi vya Urusi hivi sasa vinazidisha kampeni yake ya kuudhibiti mji wa bandari wa Mariupol, kama sehemu ya mashambulizi makali ambayo yametabiliwa katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine. Moscow inaaminika kujaribu kuunganisha eneo lililonyakuliwa la Crimea na maeneo yanayotaka kujitenga ambayo yanaungwa mkono na Urusi ya Donetsk na Luhansk huko Donbas.

Kwingineko

Meya wa mji wa Bucha ambako mamia ya miili iligunduliwa baada ya wanajeshi wa Urusi kujiondoa, amesema kwamba zaidi ya watu 400 wameuawa hadi kufikia sasa, huku wanawake 25 wakiripotiwa kubakwa. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema wachunguzi wamepokea ripoti za "mamia ya kesi za ubakaji" katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakidhibitiwa na wanajeshi wa Urusi, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji kingono dhidi ya watoto wadogo. Zelensky amewaambia wabunge wa Lithuania kwa njia ya video kwamba "Mamia ya visa vya ubakaji vimerekodiwa, vikiwemo vya wasichana wadogo na watoto wadogo sana. Hata mtoto mchanga!"

Moja ya jengo la makaazi ya raia lililoharibiwa huko MariupolPicha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wametaka uchunguzi ufanyike kuhusiana na matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake ambayo yamemkasirisha rais Zelensky. Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema zaidi ya wakimbizi milioni 4.6 wa Ukraine sasa wameikimbia nchi, huku asilimia 90 kati yao wakiwa wanawake na watoto.

Silaha za Kemikali

Hayo yakiripotiwa shirika la udhibiti wa matumizi ya silaha za kemikali duniani OPCW limeelezea wasiwasi juu ya "ripoti ambazo hazijathibitishwa" za matumizi ya silaha za kemikali mjini Mariupol na kusema kwamba linafuatilia kwa taarifa hizo. Katika taarifa yake, shirika hilo limesema "matumizi ya silaha za kemikali popote na mtu yeyote chini ya hali yoyote ni kinyume kabisa na kanuni za kisheria zilizowekwa na jumuiya ya kimataifa dhidi ya matumizi hayo."Zelenskiy: Hatuna silaha za kutosha kuikomboa Mariupol

Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken imesema kuwa ina "taarifa za kuaminika" kwamba Urusi "inaweza kutumia silaha za kemikali" katika mashambulizi yake kuudhibiti mji wa Mariupol. Blinken hata hivyo aliongeza kwamba hawezi kuthibitisha tuhuma kwamba Moscow tayari imetumia silaha hizo. Rais wa Marekani Joe Biden kwa mara ya kwanza ameutaja uvamizi wa Urusi kama "mauaji ya halaiki,'' yanayohusisha vita na kupanda kwa bei.

Wakati huohuo Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema Ukraine imekataa kiongozi huyo kuzuru Kyiv.Steinmeier amedai kwamba alijitolea kuzuru Ukraine pamoja na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya lakini aliambiwa na Kyiv safari yake "haitakiwi". Steinmeier, waziri wa zamani wa mambo ya nje chini ya utawala wa kansela wa zamani Angela Merkel, alijulikana kwa muda mrefu kwa kutetea uhusiano na Moscow. Kashfa hiyo inakuja wakati Kansela Olaf Scholz anakabiliwa na shinikizo kubwa la kutotembelea Ukraine.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW