1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aongoza katika majimbo muhimu, Georgia na Pennsylvania

6 Novemba 2020

Mgombea urais wa Marekani wa chama cha Democratic Joe Biden amechukua uongozi wa kura katika jimbo la Georgia. Jimbo hilo ni miongoni mwa majimbo yaliyosalia na yenye ushindani mkali.

US Wahl 2020 Joe Biden
Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Hayo yakijiri ripoti za vyombo vya habari Marekani zinasema Biden anatarajiwa kuongezewa maafisa wa ulinzi.

Kwamba Joe Biden amechukua uongozi katika jimbo la Georgia haimaanishi moja kwa moja kuwa ameshinda katika jimbo hilo hasa ikizingatiwa tofauti ya kura kati yake na Trump ni chini ya 1,000.

Lakini ikiwa Biden atashinda katika jimbo hilo ambalo limekuwa ngome ya chama cha Republican tangu mwaka 1992, iliyo na jumla ya kura maalum 16, na pia apate ushindi katika jimbo la Arizona, basi bila shaka atakuwa amefikisha jumla ya kura maalum 270, ambazo mgombea lazima apate na zaidi ndipo aibuke mshindi.

Soma pia: Biden apata kura zaidi Georgia

Hadi sasa Biden anaongoza kwa jumla ya kura maalum 264 kwa mujibu wa ujumuishaji wa shirika la habari la Associated Press huku Trump akiwa na jumla ya kura maalum 214.

Hesabu za kura zipo katika hatua za mwisho katika majimbo yaliyosalia, huku nafasi za Rais Trump kushinda zikiendelea kudidimia.

Uchaguzi wa Marekani unafuatiliwa kwa karibu ulimwenguni kote na watu wana mitazamo tofauti tofauti kuhusiana na yanayojitokeza, mfano Patrick Gathara kutoka Kenya ambaye pia ni mchambuzi wa siasa na mchoraji vibonzo.

Wasemayo Watanzania kuhusu uchaguzi Marekani

02:38

This browser does not support the video element.

''Wengi wanatizama yanayojitokeza Marekani kama kichekesho hasa kwa nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele kujionyesha kuendelea kidemokrasia na kumfundisha kila mtu kuhusu namna ya kufanya uchaguzi huru na wa haki, kisha inageuka kuwa kumbe wamekuwa wakihubiri maji huku wakinywa mvinyo.'' Amesema Gathara.

Huku hayo yakijiri baadhi ya vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti kuwa Biden anatarajiwa kuongezewa maafisa zaidi wa ulinzi, kutoka katika kikosi maalum maarufu kama ‘Secret Service'.

Soma pia: Trump adai kuwa mshindi, ila wizi wa kura

Kulingana na ripoti katika gazeti la Washington Post, maafisa zaidi wataongezwa katika makao yake yaliyoko Chase Centre mjini Wilmington, anakokaa kwa sasa pamoja na wafanyakazi wake.

Maafisa wengine pia wanatarajiwa kupelekwa kushika doria katika eneo ambako Biden anatarajiwa kutoa hotuba yake muhimu.

Msemaji wa kikosi hicho cha Secret Service alisema hawezi kuzungumzia hatua hizo za kiusalama zilizoripotiwa na Washington Post.

Maafisa wa uchaguzi katika majimbo yaliyosalia wamesema wanafanya juu chini kuhakikisha wanahesabu kila kura, huku wakiongeza kuwa mchakato huo umekawia kumalizika kwa sababu ya idadi kubwa ya watu waliopiga kura kwa njia ya posta.

Zaidi ya watu milioni 100, walipiga kura zao kupitia njia ya posta kutokana na hofu ya janga la virusi vya corona.

Haijabashiriwa nani ataibuka mshindi katika majimbo ya Pennsylvania na Nevada japo Biden anaendelea kupata kura zaidi.

Mara kadhaa, Rais Trump amedai kuwa wizi wa kura unafanywa dhidi yake, lakini bila ya kutoa ushahidi.

SOma pia: Uchaguzi wa Marekani wairarua demokrasia ya kiliberali

Katika hotuba yake akiwa kwenye ikulu ya Marekani, Trump aliwatuhumu wapinzani wake kwa kulenga kuiba kura dhidi yake.

Maafisa wa uchaguzi wakihesabu kura jimbo la PennsylvaniaPicha: Rachel Wisniewski/REUTERS

Kwa upande wake, Biden amechukua mkondo tofauti, na kuwataka watu kuwa na subira hadi kura zote zihesabiwe, na kuongeza kuwa hana shaka yoyote kuwa ataibuka mshindi.

Mnamo Alhamisi usiku, wafuasi wa Trump ambao baadhi yao walibeba bunduki waliandamana kufuatia madai ya Trump kuwa kuna wizi wa kura dhidi yake. Lakini pia kulikuwa na waandamanaji waliopinga madai hayo ya Trump. Maandamano hayo yalikuwa ya amani.

Mjini Philadelphia, polisi wamesema walimkamata mtu mmoja na pia kukamata silaha, kama sehemu ya uchunguzi wao wa madai ya kuwepo njama ya kushambulia ukumbi wa kuhesabia kura Pennsylvania.

Mtandao wa Twitter umeweka maonyo kwenye ujumbe kadhaa wa Trump kuhusu madai wizi wa kura, ukisema rais anaeneza uongo. Na kwamba hakuna afisa yeyote wa uchaguzi ameripoti kisa cha udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Rais Trump amekuwa akidai kuwa wizi wa kura unafanyika dhidi yake, lakini bila ya kutoa ushahidiPicha: Chris Kleponis/UPI Photo/imago images

Mtandao wa Facebook pia umeondoa ukurasa wa kundi moja ambalo wafuasi wa Trump walikuwa wakitumia kueneza mawazo na fikra za vurugu.

Kituo cha televisheni cha DW Kingereza, kimesema hakitaendelea kupeperusha moja kwa moja kauli za Trump kikamilifu. Badala yake kitasitisha matangazo hayo ikiwa Trump atatoa wito wa kutaka kura zisihesabiwe au endapo atatoa madai ya wizi wa kura bila ya ushahidi.

Hapo jana vyombo kadhaa vya habari nchini Marekani vilisitisha kupeperusha moja kwa moja madai ya Trump alipotoa madai ya wizi katika uchaguzi.

Vyanzo: (DPA, RTRE, APE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW