1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden: 'Karibu tuipoteze Marekani'

6 Januari 2024

Rais wa Marekani Joe Biden ameadhimisha miaka mitatu tangu uvamizi kwenye jengo la Bunge nchini humo kwa kuonya juu ya kitisho kinacholetwa na utawala wa aliyekuwa Rais Donald Trump wa chama cha Republican.

Rais Joe Biden azungumzia uvamizi wa jengo la Bunge uliofanywa na wafuasi wa aliyekuwa Rais Donald Trump
Rais Biden akizungumza kabla ya Maadhimisho ya miaka mitatu ya uvamizi wa jengo la Bunge, Januari 5, 2024.Picha: Matt Rourke/AP/picture alliance

Rais Joe Biden ametoa hotuba hiyo katika mkesha wa kumbukumbu ya uvamizi huo, Januari 6, 2021 baada ya wafuasi wa Trump kuvamia jengo la Capitol Hill ambako wabunge walikuwa wakiidhinisha ushindi wake wa urais.

Biden amesema kampeni za Trump ziligubikwa na maslahi binafsi kuliko kuwasaidia Wamarekani na kwamba rais huyo wa zamani anaweza kuitoa muhanga demokrasia ikiwa atarejea madarakani.

Biden: 'Nilishinda uchaguzi, alishindwa'

"Nilishinda uchaguzi, na alishindwa," Biden alisema, "Alibakiwa na chaguo moja, machafuko ya Januari 6."

Rais huyo wa sasa wa Marekani amesema uvamizi katika jengo la Capitol ulikuwa ni "siku ambayo wangekaribia kuipoteza Marekani."

Soma pia: Biden amlaumu Trump kwa uvamizi wa Capitol

Biden ametoa hotuba hiyo katika eneo la Valley Forge, ambako kihistoria panarudisha kumbukumbu ya mahali ambako aliyekuwa rais George Washington na jeshi la muungano wa Makoloni "Continental Army" walikaa kwa miezi sita chini ya mazingira magumu na baridi kali wakati wa vita vya Mapinduzi ya Marekani miaka 250 iliyopita. Biden alizungumzia juu ya vitisho dhidi ya demokrasia, baada ya majadiliano na wanahistoria na wasomi katika Ikulu ya White House

Donald Trump akiwa Iowa - Desemba 19, 2023**Rais wa zamani wa Marekani na mgombea urais wa 2024 Donald Trump alipomaliza mkutano wa kampeni huko Waterloo, Iowa, Desemba 19, 2023.Picha: Kamil Krzaczynski/AFP/Getty Images

Biden amesema kwambaTrump aliyasifu machafuko hayo ya Capitol yaliyosababisha watu karibu tisa kufa, ama wakati wa machafuko au baada ya kisa hicho na kuongeza kuwa "kwa kuangazia tukio hilo la Januari 6, Trump anajaribu kuiiba historia kana alivyojaribu kuiba kura."

"Kampeni za Donald Trump zilikuwa ni kwa ajili yake, " alisema Biden akiiangazia mipango ya Trump ya kulipiza kisasi dhidi ya maadui zake wa kisiasa ikiwa atarejea ikulu ya White House. "Sio Marekani. Sio wewe. Kampeni za Donald Trump zinazungumzia tu yaliyopita, na sio ya siku za usoni."

Biden dhidi ya Trump; awamu ya pili

Bado haiko wazi ikiwa maonyo hayo ya Biden yatakuwa na matokeo yoyote kwa wapiga kura wakati kampeni za urais zikianza.

Biden alimshinda Trump kwa asilimia 51.3 ya kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, lakini ongezeko la mfumuko wa bei na wasiwasi kuhusiana na umri wake mkubwa kwa pamoja vinaibua mashaka hata zaidi kwa wafuasi wake.

Trump kwa upande wake anatarajia kufanya mkutano wa hadhara huko Iowa siku ya Jumapili.

Soma pia: Trump apigwa marufuku kushiriki uchaguzi wa mchujo katika jimbo la Maine

Trump anakabiliwa na msururu wa kesi, ikiwa ni pamoja na madai ya kuhusika kwake katika ghasia za Januari 6, mashtaka ya kuingilia uchaguzi wa 2020 katika jimbo la Georgia, na mashtaka ya kushughulikia vibaya nyaraka za siri zilizopatikana nyumbani kwake.