1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden arai Wamarekani kuzika tofauti za wakati wa uchaguzi

8 Novemba 2024

Rais Joe Biden wa Marekani amewatolea mwito Wamarekani "kupunguza joto la kisiasa" na kumaliza tofauti za wakati wa uchaguzi ambao umempa ushindi mwanasiasa wa Republican na rais wa zamani, Donald Trump.

Rais Joe Biden wa Marekani
Rais Joe Biden wa Marekani.Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Kwenye hotuba yake aliyoitoa kwenye viunga vya ikulu ya White House siku mbili tangu kumalizika uchaguzi, Biden amewahimiza Wamarekani kuwa na mshikamano bila kujali upande walioupigia kura katika uchaguzi wa Novemba 5.

Biden ametumia hotuba hiyo pia kuwarai wanachama wa chama chake cha Democratic "kutokata tamaa" baada ya mgombea wao Kamala Harris kupoteza kinyanganyiro cha urais.

Ama kuhusu mipango ya kukabidhi madaraka kwa utawala mpya wa Trump, Biden ameahidi mchakato huo utafanyika kwa njia ya amani na desturi zilizozoeleka nchini humo.

Kiongozi huyo pia amemkaribisha Rais Mteule Trump kwa mazungumzo kwenye ikulu ya White House, utamaduni uliozoeleka kati ya rais anayeondoka na yule anayejiandaa kuingia madarakani.