Biden aridhia uwepo wa wanajeshi wa Marekani Somalia
17 Mei 2022Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani John Kirby, amesema kwamba Biden aliridhia ombi la wiazara hiyo kuwahamisha wanajeshi wa Marekani katika eneo la Afrika Mashariki ili kurejesha tena idadi ndogo ya jeshi la Marekani katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika.
Kwa mujibu wa afisa huyo vikosi visivyozidi 500 vitapelekwa, na kwamba itachukua muda kufikia kiwango hicho kuelekea nchini Somalia.
Hatua hiyo inabatilisha amri ya mtangulizi wa Biden, rais wa zamani Donald Trump ambaye mwishoni mwa 2020 aliviondoa vikosi karibu vyote kutoka nchi za Afrika Mashariki alipotaka kufikisha mwisho harakati zote za kijeshi za Marekani nje ya nchi wakati wa wiki zake za mwisho madarakani.
Usalama zaidi
Kirby aliashiria kwamba uamuzi wa Biden unahusiana zaidi na usalama wa vikosi vya Marekani kuliko uchaguzi wa rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa Jumapili iliyopita baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa migogoro ya kisiasa na mgogoro wa ukame.
"Wamekuwa na uwezo wa kufanya mashambulio katika kanda hiyo.Na tunajua katika kipindi cha nyuma wamekuwa wakizungumzia alau dhamira ya kutaka kushambulia nje yaeneo hilo ikiwa ni pamoja na, na dhidi ya maslahi ya Marekani. Kwahiyo tunalifuatilia hili kwa makini. Hilo sio tishio litakalokwisha.Tena sio kama hatujafanya lolote Somalia. Sio kweli. Ni waziri wa ulinzi tu anaamini na rais ameridhia pendekezo kwamba njia bora zaidi ya kufikia tishio hilo ni kuwa na uwepo wa kudumu zaidi. Lakini itakuwa ni uwepo wa wastani. Na kwamba kazi tunayofanya itakuwa makini kwa tishio hilo." amesema Kirby.
Marekani itapambana na tishio
Viongozi wa Somalia katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakiunga mkono mara kwa mara ushirikiano wao na jeshi la Marekani katika kupambana na wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali. Aidha afisa wa Marekani ameongeza kuwa Washington inasalia kuwa na imani kwamba utawala mpya utaendelea kufanya hivyo.
Kwa kuwarejesha tena wanajeshi wa Marekani, Washington itapunguza hatari zinazohusika katika uhamasishaji wa kurudi kwa vikosi ambavyo vimekuwa vikiendesha operesheni za kukabiliana na ugaidi ndani ya Somalia.
//AFP