1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden asema Iraq imepiga hatua

13 Januari 2011

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden amewasili mjini Baghdad kwa mkutano wa kwanza na Nuri al Maliki tangu waziri huyo mkuu wa Iraq kuanza hatamu yake ya pili.

Makamu wa rais Joe Biden aliwasili Baghdad jana usikuPicha: AP

Biden yuko katika ziara ya ghafla katika maeneo ya vurugu kubwa duniani. Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden, amewasili Iraq baada ya kuzizuru Afghanistan alikokutana na rais Hamid Karzai na nchini Pakistan ambako alikua ana mazungumzo na maafisa wakuu wa serikali ya nchi hiyo.

Hii leo asubuhi Joe Biden alikutana na kamanda mkuu wa jeshi la Marekani Iraq, jenerali Lloyd Austin na balozi wa Marekani James Jeffrey katika katika ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.

Alipoulizwa ni kwa nini amefika nchini humo, Biden alisema kuwa amefika kuwasaidia Wairaqi kusherehekea hatua walioipiga ya kuunda serikali kwani ni jambo zuri na wana njia ndefu inayowasubiri.

Kwa mujibu wa waandishi wa habari wanaosafiri naye, Biden amewasili mjini Baghdad hapo jana usiku kutoka Pakistan.

Ikulu ya Marekani imesema kwamba makamu huyo wa rais pia atakutana na rais Jalal Talabani na mkuu wa chama cha Iraqiya na aliyeshinda kura nyingi katika uchaguzi wa mwaka uliopita nchini humo, Iyad Allawi.

Ushawishi wa Marekani Iraq

Kuna wanajeshi 50,000 wa Marekani nchini IraqPicha: AP

Ziara hii ya Biden inajiri siku moja baada ya kiongozi wa dhehebu la kishia mwenye itikadi kali, Moqtada al Sadr aliye na shinikizo kubwa katika siasa za nchi hiyo, kutoa wito mkali kwa wananchi kukaidi uwepo wa Marekani kwa njia zozote. Aliyasema haya katika hotuba yake ya kwanza tangu kurudi nyumbani katika mji mtakatifu wa Najaf.

Maliki aliidhinishwa na bunge mwezi Desemba tarehe 21, kushikilia wadhifa wa waziri mkuu kwa awamu ya pili pamoja na baraza la mawaziri la serikali ya umoja wa taifa, baada ya mkwamo wa kisiasa wa muda wa miezi tisa.

Ijapokuwa operesheni za kivita zimekwisha nchini humo, kiasi ya wanajeshi elfu 50 wa Marekani wakalipo nchini Iraq ambapo wanaruhusiwa kulipiza mashambulio katika kujilinda, na wanaruhusiwa kushiriki katika operesheni iwapo wataombwa na wanajeshi wenzao wa Iraq kwa mujibu wa makubaliano ya pamoja ya kiusalama.

Kikao mjini Copenhagen

Ama kwa upande mwingine, kikao kinachokutanisha baadhi ya viongozi wakuu wa kidini wa Iraq mjini Copenhagen Denmark, unaotarajiwa kufanikiwa kupata msimamo wa pamoja wa kushutumu vurugu dhidi ya Wakristo, umeingia siku ya pili hii leo.

Mkutano huo wa dharura ulioandaliwa na taasisi ya msaada na maridhiano katika eneo la mashariki ya kati, na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Denmark, unafanyika baada ya kutokea mfululizo wa mashambulio dhidi ya Wakristo nchini Iraq na Misri.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Afpe
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW