1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden ataka China na Marekani zitanue ushirikiano

4 Desemba 2013

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, amesema China na nchi yake lazima zitanue ushirikiano wa kivitendo wenye kuonesha matokeo huku akikosoa mfumo wa elimu na utawala wa China.

Makamu wa Rais wa Marekani akianza ziarani nchini China.
Makamu wa Rais wa Marekani akianza ziarani nchini China.Picha: picture-alliance/dpa

Biden amewasili China mapema leo, alikopokelewa kwa gwaride la kijeshi, na kisha moja kwa moja akaelekea ubalozi wa nchi yake jijini Beijing. Ziara hiyo ya ghafla ubalozini, ilikusudiwa kuunga mkono mpango wa Marekani kupunguza vikwazo vya Wachina wanaotaka kuingia Marekani.

Biden ameliambia kundi la watu hao, wengi wao vijana, kwamba anatarajia wakati wa kutembelea kwao Marekani watajifunza kwamba uvumbuzi unakuja tu pale mtu anapopumua kwa uhuru.

"Nchini Marekani, watoto wanazawadiwa kwa kuupa changamoto mfumo uliopo na sio kuadhibiwa. Njia pekee ya kukifanya kitu kuwa kipya kabisa, ni kukivunja kikongwe." Biden aliwaambia vijana hao.

Kauli kama hii inayouokosoa mfumo wa utawala na kielimu wa China iliwahi kuzua mzozo baina ya nchi hizo mbili siku za nyuma.

Wakati Biden alipowaambia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania mwezi Mei mwaka huu kwamba huwezi kufikiri tafauti katika taifa ambalo huwezi kuvuta hewa kwa uhuru, wanafunzi wa Kichina kwenye chuo hicho walisema wametukanwa na wakataka waombwe radhi.

Mgogoro wa Bahari ya Kusini

Biden amewasili China akitokea Japan, ambako mazungumzo yake ya hapo jana na viongozi wa Japan, yalituwama juu ya hatua ya China kutangaza eneo la ulinzi wa anga katika eneo linalojumuisha visiwa vinavyozizaniwa kwenye Bahari ya Kusini. Marekani, Japan na Korea ya Kusini zinapingana vikali na hatua hiyo.

Makamu wa Rais wa Marekani akiwa nchini Japan.Picha: Reuters

Aliwaambia viongozi wa Japan hapo jana kwamba Marekani inatiwa wasiwasi sana na hatua hiyo ya China na kusema kwamba inaongeza hatari za kutokea kwa ajali, suala ambalo atalizusha leo kwenye mazungumzo yake na Rais Xi Jinping wa China.

Amekutana na Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao, kwenye jengo la Ukumbi wa Watu wa China, ambapo alisifia jitihada za Rais Xi katika kutatua tafauti zilizopo baina ya Marekani na China. Biden atakuwa na mazungumzo na Rais Xi baadaye jioni ya leo.

Na kabla ya kuondoka hapo kesho, atakuwa na mazungumzo na wafanyabiashara wa Kimarekani nchini China kwenye chai ya asubuhi na baadaye kukutana na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang. Baadaye ataelekea Korea ya Kusini ikiwa ni kituo chake cha mwisho cha ziara hii ya Asia ya Mbali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi