1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden ataka Wamarekani watulize joto la kisiasa

15 Julai 2024

Rais wa Marekani Joe Biden Jumatatu ametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kutuliza joto la kisiasa kufuatia jaribio la kumuua hasimu wake katika uchaguzi ujao Donald Trump huko Pennsylvania Jumamosi.

Marekani, Washington | Hotuba kwa taifa kutoka kwa RaisJoe Biden
Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Erin Schaff/Pool/REUTERS

Akizungumza na taifa kupitia afisi ya Oval kwenye ikulu ya White House Jumatatu, mfumo ambao hutumika kwa rais wa Marekani kulihutubia taifa wakati wa mzozo tu, Biden amesema ingawa Wamarekani wanatofautiana, si maadui.

Kiongozi huyo vile vile amewakumbusha raia wa nchi hiyo kwamba Wamarekani husuluhisha tofauti zao kupitia kura tu na wala sio mtutu wa bunduki.

Biden kwa mara nyengine amelaani tukio hilo dhidi ya Trump ambaye alipigwa risasi iliyokata sehemu ya sikio lake na kumpelekea kuvuja damu.

Donald Trump baada ya kushambuliwa wakati wa kampeniPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Trump ahudhuria mkutano mkuu wa chama cha Republican

Afisa mmoja wa zima moto aliyekuwa katika mkutano huo wa kampeni ya Trump alifariki dunia na watu wengine wawili kujeruhiwa vibaya.

Wakati huo huo siku moja baada ya kuponea hilo jaribio la mauaji,Donald Trump amewasili Milwaukee huko Marekani ambako atateuliwa rasmi kama mgombea wa urais wa chama Republican baadae wiki hii.

Jaribio hilo la mauaji limezidisha machungu yaliyopo baina ya pande zinazohasimiana kisiasa Marekani.

Trump na Rais Joe Biden wote wametoa wito wa utulivu.

Biden na Trump hawatofautiani pakubwa kulinga na tafiti za maoni

Trump siku ya Alhamis anatarajiwa kukubali uteuzi rasmi wa chama chake cha Republican katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa chama hicho.

Mkutano wa kisiasa wa trump Pennsylvania baada ya kutibukaPicha: Gene J. Puskar/AP Photo/picture alliance

Kulingana na tafiti nyingi za maoni, hakuna tofauti kubwa kati ya Trump na Biden katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania kuelekea katika ikulu ya White House.

Shambulio hilo la Jumamosi dhidi ya Trump lilipunguza moto wa gumzo lililokuwepo katika chama cha Democratic la kumtaka Rais Biden aachie ngazi kama mgombea wa urais wa chama cha Democratic kutokana na umri wake.