Biden atangaza Marekani kuanza kudondosha misaada Gaza
2 Machi 2024Biden amesema hayo katika Ikulu ya White House alipozongumza na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na kuongeza kuwa, katika siku za usoni wataungana na Jordan katika kufanikisha zoezi hilo la kudondosha misaada katika eneo hilo lililo katika mzingiro wa vikosi vya Israel.
Biden amekuwa akitoa shinikizo kwa Israel kupunguza vifo vya raia na kuruhusu misaada ya kiutu kuingia, huku akiendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa mshirika wake Israel.
Ameongeza kuwa ana matumaini na makubaliano ya usitishwaji vita kwa kipindi cha wiki sita cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao utaanza Machi 10 au 11 kulingana na muandamo wa mwezi.
Soma pia:Dunia yalaani shambulizi la Israel dhidi ya Wapalestina Gaza
Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, imesema idadi jumlya ya vifo tangu kuanza kwa vita katika eneo hilo la Wapalestina imefikia 30,320, baada ya vifo vipya 92 kurekodiwa katika muda wa saa 24 zilizopita.
Wizara hiyo imesema kwamba watu 71,533 wamejeruhiwa Gaza tangu kuzuka kwa vita hivyo Oktoba 7.