1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden atarajiwa kuhutubia taifa

7 Novemba 2024

Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuhutubia taifa siku ya Alhamisi baada ya chama chake cha Democratic kushindwa katika uchaguzi wa Jumanne, ambapo Donald Trump alifanikiwa kurejea tena madarakani.

Marekani I Washington - Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden atarajia kuhutubia taifa, kuhusu matokeo ya uchaguzi na mustakabali wa kukabidhi madaraka kwa rais mteule Donald Trump.Picha: Ron Sachs/Pool/CNPZUMA Press Wire/IMAGO

Biden anatarajiwa kutoa hotuba yake katika Ikulu ya White House, ambapo ataahidi kusaidia kipindi cha mpito kuanzia sasa hadi kuapishwa kwa Trump hapo Januari 20.

Rais huyo ambaye mgombea wake, KamalaHarris, amebwagwa vibaya na Trump kwenye uchaguzi huo, amewataka wanachama wa chama chake cha Democrat kuendelea kupigania kile wanachokiamini.

Soma pia: Biden amualika Trump katika Ikulu ya White House

Kinyume na Trump mwenyewe ambaye alikataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa 2020 na matokeo yake wafuasi wake wakasababisha vurugu katika majengo ya bunge mnamo Januari 6, 2021, katika hotuba ya leo, Biden anatazamiwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi wa juzi na muelekeo wa kipindi cha mpito kuelekea utawala mwengine wa Trump.

Mustakabali wa udhibiti wa Baraza la Wawakilishi la Marekani umegawanyika kati ya wingi wa uwakilishi wa Republican au Democratic. Lakini kufikia jana Jumatano Warepublican walikuwa wameshinda kwenye udhibiti wa Seneti.

Marekani na dunia kwa ujumla inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa baada ya ushindi wa kihistoria wa Trump. Kwa mujibu wa kura za maoni, wapiga kura wa Marekani waliunga mkono sera za Trump za mrengo mkali wa kulia na kukataa rekodi ya Biden na Harris, hasa katika masuala ya uchumi na mfumko wa bei.

Ulaya inatazama vipi ujio mpya wa Trump?

Ushindi wa kihistoria wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani umetikisa siasa za dunia.Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Kurudi madarakani kwa Trump kumebadili ajenda ya mkutano wa viongozi wa Ulaya. Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen ni miongoni mwa viongozi wa dunia wanaotarajia mabadiliko katika utawala mpya wa Marekani.

Soma pia: Viongozi wa Ulaya wakutana Budapest kufuatia ushindi wa Trump

"Kwa hivyo tutakuwa tukifanya kazi na utawala mpya wa Trump kwa njia nzuri na kuangalia kile kilicho mbele yetu. Nina uzoefu wa kufanya kazi na Rais Trump alipokuwa madarakani mwanzoni."

"Kwa hivyo kuna mahala pa kuanzia. Na nadhani muhimu sana ni kwamba tuchambue pamoja  masilahi yetu ya pamoja na kuyafanyia kazi."

Katika kuunda timu yake ndani ya Ikulu ya White House, Trump anatatajiwa kumjumuisha bilionea na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa X, Elon Musk, na aliyekuwa mgombea binafsi kwenye uchaguzi wa jusi, Robert F. Kennedy Jr.

Trump amehidi kufanya mabadiliko kuliko ilivyokuwa katika muhula wake wa kwanza na anaweza kuondosha sehemu kubwa ya yale yaliyofanywa na Biden. Huenda akaanza kwa kusitisha mabilioni ya dola za msaada wa kijeshi kwa vita vya Ukraine dhidi ya Urusi.

Soma pia: Upi mtazamo wa Trump kuelekea Afrika?

Trump pia atarejea Ikulu ya White House kama kiongozi anayepinga dhana ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa, akiwa tayari kutengua sera za ulinzi wa mazingira za Biden.