1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden ayafuta maagizo ya Trump juu ya mazingira na uhamiaji

Daniel Gakuba
21 Januari 2021

Rais mpya wa Marekani Joe Biden amesaini mlolongo wa maagizo ya kiutendaji yanayobatilisha mengine yaliyoewekwa na mtangulizi wake, Donald Trump. Baadhi yanahusu mazingira, uhamiaji na mapambano dhidi ya COVID-19.

USA Washington | Inauguration | Joe Biden im Oval Office
Rais Joe Biden wa Marekani akilisaini mojawapo ya maagizo ya kiutendajiPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Kwa kuyasaini maagizo hayo Rais Biden amedhamiria kuonyesha mabadiliko makubwa ya mwelekeo wa siasa za Marekani. Mshauri wake kuhusu magonjwa ya miripuko, Dr Anthony Fauci ameuhutubia kwa njia ya video mkutano wa shirika la Afya ulimwenguni WHO, na kuarifu kuwa Marekani inajiunga na ushirika wa kidunia kwa ajili ya chanjo kwa wote.

Soma zaidi:  Viongozi duniani wampongeza Biden na Kamala

Aidha, Dr Fauci ameahidi kuwa Marekani itarejea tena katika shirika la WHO kama mwanachama.

''Ninayo fahari kutangaza kuwa Marekani itabakia kuwa mwanachama wa WHO. Jana Rais Joe Biden alisaini barua inayofuta tangazo la kujiondoa katika shirika hilo, na barua hiyo tayari imetumwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kwako Dr Tedros, rafiki yangu.'' Amesema Dr Fauci katika mkutano huo.

Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo kutokana na COVID-19Picha: Jae C. Hong/AP Photo/picture alliance

Tedros Adhanom Ghebreyesus ni mkurugenzi mkuu wa WHO ambaye mwaka jana alikosolewa vikali ya Donald Trump, kabla ya rais huyo aliyepita wa Marekani kuiondoa nchi yake katika shirika la afya ulimwenguni, alilolituhumu kushindwa vibaya katika mapambano dhidi ya janga la corona. Dr Fauci pia alithibitisha kuwa Marekani inarejesha ufadhili wa kifedha kwa shirika hilo.

Mchaka-mchaka kupambana na COVID-19

Agizo la kujiunga tena na WHO, pamoja na kurejea katika makubaliano ya kimataifa ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa maagizo 17 aliyosaini Biden mnamo siku yake ya kwanza madarakani.

Soma zaidi:  Biden kusaini maagizo ya kiutendaji baada ya kuapishwa

Na leo hii rais huyo anatarajiwa kuyasaini mengine 10, yanayohusu moja kwa moja mapambano dhidi ya janga la COVID-19 ambalo limeambukiza Wamarekani zaidi ya milioni 24.5, na kuwauwa wasiopungua 400,000.

Tedros Adhanom Ghebreyesus, shirika la afya ulimwenguni analoliongoza (WHO) lilipata wakati mgumu chini ya utawala wa Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/KEYSTONE/S. D. Nolfi

Maagizo hayo ya kiutendaji ni pamoja na ulazima wa kuvaa barakoa katika majengo yote ya serikali ya shirikisho, na kutumia sheria ya uzalishaji wa kiulinzi kuwezesha utengenezaji wa vifaa vya kutosha kuwakinga watu dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Dunia yashusha pumzi ya ahueni

Viongozi wengi muhimu duniani wamesifu mwelekeo mpya wa Marekani baada ya Trump kuondoka. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema leo kuwa kwa kuzingatia maagizo aliyoyasaini Biden, ni wazi kuwa wigo wa ushirikiano baina ya Marekani na Ujerumani umepanuka.

Soma zaidi:  Biden azindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema vipaumbele vya Rais Joe Biden vinashabihiana na vile vya Uingereza, vikiwemo ulinzi wa mazingira na mapambano dhidi ya virusi vya corona.

China, ambayo ilikabiliwa na mbinyo mkali wa Marekani chini ya uongozi wa rais Donald Trump, imesema kupitia wizara yake ya mambo ya nje, kuwa inatazamia kuboreka kwa mahusiano baina ya mataifa hayo mawili yanayoongoza kiuchumi duniani, na ushirikiano katika kuzishughulikia changamoto zinazoikumba dunia.

Vyanzo: ape, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW